Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limezidi kuandamwa
na kashfa, kutokana na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa
juzi kuwa mabaya.
Kashfa hiyo inazidi kuchukua sura mpya kutokana na
udanganyifu mkubwa, ambapo imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi waliopata alama
za juu katika matokeo hayo hawakufanya mitihani.
Taarifa hizo ziliibuliwa jana na Mkurugenzi wa Shule ya
Sekondari ya Green Acres, Julian Bujugo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam juu ya matokeo hayo.
Bujugo, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Magomeni, jijini
Dar es Salaam, alionyesha kukerwa na matokeo hayo, huku akihoji mazingira ya
baadhi ya wanafunzi wa shule yake kupatiwa alama za juu.
Katika mazungumzo yake, Bujugo alisema wanafunzi wa shule
yake wamefanyiwa mchezo mchafu na baadhi ya watendaji wa Baraza la Mitihani
nchini, jambo ambalo limewaathiri kisaikolojia.
Bujugo alisema katika matokeo hayo, wanafunzi wake watatu
wamekumbwa na tatizo hilo ambapo mmoja wa wanafunzi hao, Amphey Sanga,
aliyefukuzwa shuleni hapo kabla ya kufanya mitihani, alionekana kufanya vizuri
kwa kupata daraja la tatu na pointi 24 (Div 3 ya pointi 24)
“Baada ya kupata matokeo haya, tumefanya uchambuzi wa
haraka ambapo mwanafunzi Amphey Sanga amepewa namba ya mtihani 01197/0148.
“Matokeo yake amepata masomo ya Civics- D, Historia-D,
Geograph-C, Kiswahili-D, Kiingereza-C, Physics-D, Chemistry-C, Biology-C na
Hesabu-D, ambapo amepata Division 3.24.
“Tunashangaa huyu mwanafunzi amepataje alama hizi hali ya
kuwa hakufanya mtihani wa Taifa na alifukuzwa hapa shuleni?,” alihoji Bujugo.
Matokeo mengine yanayoleta utata na kushangaza ni kuhusu
mwanafunzi aliyefanya mtihani huo wa taifa, Martin Rushwangwa, mwenye namba ya
Mtihani 01197/0173, ambaye matokeo yake yanaonyesha amepata daraja sifuri.
Mkurugenzi huyo alisema mwanafunzi huyo alisaini kufanya
masomo saba ya mchepuo wa sanaa, lakini katika matokeo yake anaonekana pia
amefanya masomo ya biashara kinyume cha utaratibu na sheria za mitihani.
Alisema mwanafunzi Habib Ibrahim naye alifanya mtihani
huo wa Taifa, lakini katika matokeo hayo inaonyesha kama hakufanya mtihani huo,
jambo ambalo sio la kweli.
“Kutokana na utata huu, hatuwezi kukubaliana kabisa na
matokeo yaliyotangazwa na kwamba kuna haja ya Wizara ya Elimu kuingilia kati
jambo hili haraka, ili haki itendeke kwa kila mmoja.
“Kwa matokeo haya, ni hakika hawakutenda haki na mfumo
wao mpya wa kusahihisha mitihani kwa kutumia namba pekee umehujumiwa.
“Tunataka usahihishaji wa matokeo ya wanafunzi wetu
urudiwe upya. Kwani hali hii imewafanya wanafunzi wengi kuathirika kisaikolojia
kwa matokeo haya ya uongo yaliyotolewa na NECTA,” alisema Bujugo.
Hali hiyo imezua taharuki kwa wanafunzi wa shule ya Green
Acres, jambo lililowafanya baadhi ya wazazi kulazimika kufika shuleni hapo na
kupanga kuitisha kikao cha dharura Jumapili ijayo ili kujadili hali hiyo.
“Jumapili wazazi watakutana hapa shuleni kwa ajili ya
kujadili hali hii na hata kutokana na uchambuzi wa matokeo ambayo bado
yanaendelea kuchambuliwa, ninatumai mambo mengi tutayabani kutokana na
uchakachuaji huu wa matokeo ya wanafunzi wa shule yetu.
“Katika hili nipo pamoja na wazazi na kubwa tunabaki na
msimamo wetu wa kutaka ni lazima usahihishaji urudiwe na kwa gharama za baraza
lenyewe. Huu ni ukandamizaji na uchakachuaji wa wazi ambapo haulipeleki Taifa
letu pazuri,” alisema.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa NECTA alippo jaribu
kuatafutwa ambaye ni Mh. John Nchimbi alitaka apewe muda wa dakika 30 ili kuweza
kupata ufafanuzi wa jambo hilo kwa kina.
Baada ya muda huo kuisha alisema kuwa hakuna kitu kama hicho, kwani NECTA imekuwa
makini katika mfumo wa usahihishaji na madai ya shule hiyo hayana ukweli
wowote.
“Swali moja katika mtihani husahihishwa na mwalimu mmoja,
sasa inawezekana vipi kwa mtu ambaye hakufanya mtihani apewe maksi, hili halipo
na hata ukiangalia mtandao wa NECTA umeweka wazi kila kitu,” alisema Nchimbi.
Post a Comment