Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka
wa pili Kitivo cha Sheria, ambaye amefahamika kwa jina moja la Joseph mwenye umri kati 22_25, amejinyonga kwa
kutumia kamba na kukutwa ameifunga juu ya mti, katika eneo la Yombo chuoni
hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Utawala, Profesa Yunus Mgaya,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kwamba alipata taarifa hizo jana asubuhi.
Aliongeza kuwa Jumamosi iliyopita alipokea simu kutoka
kituo cha polisi cha chuo hicho akielezwa kuwa kuna mwanafunzi alitishia
kujiua, lakini aliwahishwa hospitali na kupatiwa ushauri kutoka kitengo maalum
cha washauri wa chuoni hapo na kuruhusiwa Jumapili.
“Nilikuja tena kushituka leo asubuhi napokea simu kutoka
kwa mshauri wa wanafunzi kuwa kuna wanausalama wamemkuta mwanafunzi akiwa
amejinyonga juu ya mti huku akiwa na karatasi kwenye mfuko wa sharti
ikimtambulisha pamoja na ujumbe uliosema, kifo chake kisihusishwe na mtu yeyote
kwani amejiua kwa ridhaa yake --asisumbuliwe mtu yeyote kwani nimefanya hivi
kwa maamuzi yangu mwenyewe pia nizikwe kwetu--” alisema.
Profesa Mgaya alisema taratibu za mazishi zinaendelea
kufanywa na Uongozi wa chuo kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu na kwamba
Chuo kitagharamia kuusafirisha mwili kama alivyoomba katika ujumbe aliouacha wa
kupelekwa wilayani Ludewa Mkoa wa Iringa.
Naye rafiki wa marehemu, Daniel Mwamlima, alisema
marehemu hakuwahi kuzungumza chochote kilichoashiria kuwa ana matatizo wala
mgogoro na mtu yeyote. Alisema
walimuacha hospitalini Jumamosi na kesho yake kumchukua, lakini baadaye aliwatoroka.
“Sasa leo (jana) asubuhi tulipata taarifa za mwanafunzi
kujinyonga mbaya zaidi tukakuta ni yeye,” alisema Mwamlima.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho
(DARUSO), Yasini Athumani, alisema wamezipokea taarifa hizo kwa masikitiko
makubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela,
alithibitisha kutokea kwa tukio na alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba
marehemu aliwahi kuwa na historia ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa wa msongo wa mawazo.
Pia mwanafunzi aliacha ujumbe wa karatasi na kusema
asilaumie mtu.
Post a Comment