Tabia ya utoro bungeni imejirudia tena mwaka huu wakati
Bunge likijadili Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Safari hii
utoro huo unawahusisha mawaziri na siyo wabunge.
Tukio kama hilo liliwahi kutokea Julai 22, mwaka jana
wakati wa mjadala wa Bajeti wa Wizara hiyo kiasi cha kufanya moja ya vikao
vyake kuahirishwa kutokana na utoro wa wabunge.
Kutokana na utoro huo, jana asubuhi, Mbunge wa Mwibara
(CCM), Kangi Lugola alilazimika kuomba mwongozo kwa Naibu
Spika, Job Ndugai ili aone haja ya kusimamisha mjadala wa Wizara ya Kilimo
kutokana na idadi ndogo ya mawaziri waliokuwamo ukumbini.
Lugola alisema Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika ni mtambuka kutokana na kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania na
kwamba kutokana na nchi kukabiliwa na tatizo la chakula hivi sasa,
inapojadiliwa inahitaji umuhimu wa kipekee.
Mbunge huyo, ambaye amejizolea sifa ya kuihoji Serikali
bila ya woga alisema katika kipindi hicho, kulikuwa na mawaziri watano na
manaibu watano pekee ukumbini.
Baraza la Mawaziri linaundwa na mawaziri 56, ambao ni
Waziri Mkuu, mawaziri 30 na manaibu waziri 25.
“Wizara hii ni mtambuka lakini kuna mawaziri 10 pekee
humu ndani, wakiwamo mawaziri watano na manaibu watano, hivyo Mheshimiwa Naibu
Spika naomba mwongozo wako kama ni sawa kuendelea na mjadala huu katika hali
hii,” alisema Lugola.
Hata hivyo, mwandishi wetu aliwashuhudia mawaziri 13
ukumbini humo wakati huo ambao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji
na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi),
Celina Kombani na Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza.
Manaibu Waziri waliokuwamo ni Angela Kairuki (Katiba na
Sheria), Stephen Masele (Nishati na Madini), Dk Binilith Mahenge (Maji), Aggrey
Mwanri (Tamisemi), Saada Mkuya (Fedha) na Goodluck Ole-Medeye (Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi).
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika, Ndugai alisema
mawaziri wote wapo Dodoma hata kama hawakuwamo ukumbini wakati huo na walikuwa
wanashughulika na mambo mbalimbali ya bajeti zao.
“Mawaziri wote wapo Dodoma wanaweka mambo yao sawa, ili
wakija hapa wasipate shida, lakini niwaambie tu kuwa wanafuatilia kwa karibu
kila kitu kinachoendelea hapa,” alisema Ndugai.
Akihitimisha kipindi cha asubuhi cha Bunge baadaye jana,
Ndugai alisisitiza umuhimu wabunge kuhudhuria kipindi cha jioni kwa kuwa wizara
hiyo ilikuwa inahitimisha mjadala huo.
Historia yajirudia
Julai 22 mwaka jana, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia
alisimama kuomba mwongozo wa Naibu Spika, Job Ndugai kutokana na Bunge kutokuwa
na nusu ya wabunge wote kinyume cha Kanuni ya Bunge wakati wa Bajeti ya Wizara
hiyo ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Idadi ya wabunge wote ni 352 lakini wabunge waliomo humu
ndani haizidi 110, ambapo nusu ya wabunge wote ni 176 hivyo kuendelea kupitisha
bajeti hiyo ni kuvunja kanuni,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi.
Baada ya kujiridhisha kwamba idadi hiyo ilikuwa ndogo,
Naibu Spika aliahirisha kupitishwa kwa Bajeti hiyo.
Oktoba 29, 2012 utoro wa wabunge ulikwamisha kupitishwa
kwa Azimio la Marekebisho ya Pili ya Mkataba wa Ushirikiano Kati ya Jumuiya ya
Nchi za Ulaya na Nchi za Afrika, Caribean na Pacific (ACP).
Post a Comment