Onesmus Mwangi



Kijana mfanyakazi wa shambani ambaye ameunda ndege aina ya 'helikopta’ sasa anaitaka Serikali kumsaidia kufanikisha ndoto yake ya kupeperusha angani badala ya kumzima.
Bw Onesmus Mwangi, mwenye umri wa miaka 20, amekosa kifaa kimoja tu na kibali cha serikali kwa ndege yake kupaa angani.


Aidha, anahitaji cheti cha wasimamizi wa safari za ndege kupata idhini ya kupeperusha kifaa chake katika anga ya Kenya.
Ni ndoto ambayo imebakia padogo kutimia kwa kijana huyo aliyekatiza masomo kwa sababu ya umaskini. Alikosa kuendelea zaidi ya darasa la sita kwa kukosa karo.
Aidha, mamake alimkazia mara kwa mara kuunda vitu kama hivyo. Asitake mwanawe kukwama njiani na kufedheheka kwa kukosa ufadhili wa kununua vifaa alivyohitaji.
“Imewahi kupaa japo mara moja tu na hata mwenyewe sikubaini. Nilikuwa nikifanya majaribio kama kawaida nikagundua niko juu naona tu mabati ya nyumba,” aliambia Taifa Leo pia sisi tulipofika kushuhudia.
Ni ubunifu uliovutia mamia ya wakazi katika boma la tajiri wake Esther Wanjeri eneo la Magomano mjini Githunguri kijana alipowaita watu kujionea mradi wake ukifanyika halisi.
Ilibidi bikizee huyo kuwaita maafisa wa utawala kwa woga kwamba ujuzi wa kijana huyo umepita mipaka. Aidha, alihofia umati uliofurika bomani kwake kwani walifurika hadi nje na kufunga barabara.
Ni hatua hiyo iliyomfanya kuwa maarufu kwani ndege hiyo kwa sasa imepelekwa katika ofisi za mkuu wa wilaya.
Ilimchukua Mwangi miezi minane kuunda kifaa hicho – tangu Agosti mwaka jana. Hana mafunzo yoyote ya kiufundi. Kisomo chake cha darasa la sita hakijamfaa.
Ndege hiyo sio ubunifu wa kwanza, asema. Ameunda simu lakini vifaa vikamkosa. “Mamangu pia alinizuia kuunda vitu kama hivi akisema hana pesa za kuninunulia vifaa nilivyohitaji,” alideleza.
Ni mtoto wa sita kati ya watoto 12 katika familia ambayo mamake ndiye mlezi pekee.
Aliamua kutoka kwao Nyandarua kuja tafuta kazi ya kuchunga ng’ombe na ndipo akakutana na bikizee Wanderi. Kumbe alikuwa na mengine kapuni. Bi Wanderi amekuwa wa msaada sana kumtia moyo na kumadisia senti zilipomkosa.
Injini
Ni ndege iliyo na sehemu zote za kimsingi: mtaimbo endeshi, vyuma vya kusimama chini, injini japo ni ya kawaida ya gari , na yatumia mafuta ya dizeli kuguruma.
Lakini ni hilo tu aweza kufanya—kugurumisha, kwani amepewa onyo kali dhidi ya kuipeperusha angani hadi ikaguliwe na wataalamu wa serikali na kupata kibali cha mamlaka ya safari za ndege ili kufanyiwa 'majaribio’.
Kwa jumla ametumia takriban Sh57,000 hadi sasa ambazo zimekuwa ni mshahara wake tangu kuajiriwa na Bi Wanjeri.
Bidii yake ya kazi ilimtoa Sh2,000 kwa mwezi hadi Sh3,000 sasa. Alizihifadhi kwa simu kupitia Mpesa hadi zilipofika Sh10,000 zikawa mtaji wake.
“Nilianza kwa kununua vifaa vya kimsingi kama mabati, vyuma na misumari nikaunda bodi kwanza kisha nikanunua injini,” alisema kando ya ndege yake.
Anatumia mabati mepesi na vyuma vya pua: “sikuwa na pesa za kununua vyuma vya alumini.”
Anatumai wafadhili watavutiwa na ubunifu wake na kumwezesha kupata vifaa bora ili ndege yake itoshane na zile za kisasa. Yahitaji viti ndani, taa, bodi ya kisasa, mashine za kusoma mwendo na kuonyesha vipimo vingine na kadhalika.
Ukosefu wa fedha, asema hata hivyo, halitamzuia kubuni vifaa vingine. “Sasa nataka kuunda vitu vitakavyofaa watu wengi kwa pamoja,” alisema bila kufafanua.
Naam, ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.

Post a Comment

 
Top