Mwalimu Elizabeth Mmbaga, 22, aliyekutwa amefariki dunia chumbani kwake Kimara Baruti jijini Dar, Aprili 15 mwaka huu.
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa, kifo cha mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Atlas ya jijini Dar kimezua utata kutokana na jinsi mwili wake ulivyokutwa na kusababisha minong’ono ya kwamba amenyongwa na mfanyabiashara mmoja wa Kihindi (jina halikuweza kupatikana mara moja) ambaye alikuwa mpenzi wake. Uchunguzi umeonyesha kuwa, Aprili 14, mwaka huu Jumapili usiku, Mhindi mmoja alionekana akiwa na Elizabeth maeneo ya jirani na nyumbani kwa marehemu.
“Siku hiyo tulimuona marehemu akiwa na yule Mhindi baa wakinywa vinywaji karibu kabisa na alipokuwa akiishi Eliza na ilipofika usiku, wawili hao  waliondoka pamoja.
“Kesho yake ndiyo tukasikia Eliza amekutwa akiwa amekufa chumbani kwake, kimsingi kama yule Mhindi atapatikana anaweza kuisaidia polisi kwani inavyoonekana anahusika na kifo hicho,” kilidai chanzo hicho kinachoishi jirani na marehemu.
Mmoja wa marafiki wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, mara kwa mara amekuwa akiwasuluhisha Eliza na mpenzi wake huyo chanzo kikiwa ni mambo ya mapenzi na kwamba hakujua kama ugomvi huo ungeishia kwenye kifo.
“Kwa kweli inasikitisha, Eliza na yule mpenzi wake walikuwa wakigombana sana, chanzo ni haya haya mambo ya mapenzi. Nilidhani ni kutofautiana kwa kawaida tu lakini sikujua mwisho utakuwa mbaya,” alisema rafiki huyo wa marehemu.
Akazidi kudai kuwa, Mhindi huyo ambaye ni mfanyabiashara alikuwa akitaka kumuoa Eliza lakini tatizo likawa tofauti za kidini ambapo mwanaume huyo aliumia kumkosa na ikadaiwa huenda ndiyo chanzo cha mauaji hayo.
Chanzo kingine kikadai kuwa, Mhindi huyo siku chache kabla ya tukio alimdanganya Eliza kwamba muda wake wa kuishi hapa nchini umeisha hivyo kumtaka waonane ili waagane na amuachie fedha za matumizi.
“Inavyoonekana marehemu alimuamini Mhindi huyo na kuamua kwenda kuonana naye bila kujua kuwa ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya uhai wake.
“Mbaya zaidi baada ya Eliza kukutwa amekufa, pembeni zilikutwa simu zake tatu ambapo moja ilikuwa na ujumbe unaoonesha ulitoka kwa jamaa huyo akisema ametimiza alichotaka na ameondoka zake.”

Mwili wa mwalimu huyo aliyekuwa maarufu kwa jina la Ticha Eliza ulikutwa na walimu wenzake waliokwenda kumwangalia nyumbani kwake ukiwa chumbani juu ya kitanda huku chaga zikiwa zimevunjika.
“Tulilazimika kwenda nyumbani kwake baada ya kumpigia simu na ikawa inaita bila kupokelewa,” alisema mmoja wa walimu hao aliyeomba jina lake lisitajwe na kuongeza:
“Ndani ya chumba tulikuta vitu vimevurugika huku mwili wa marehemu ukionekana kuwa na alama shingoni na kwamba vitu vilivyokuwa chumbani humo vilikuwa vimevurugika, hali iliyoashiria kulikua na ugomvi au nguvu kubwa kutumika wakati wa mauaji.”

Mwalimu Mkuu, Moses Kyambo wa shule ya Atlas akizungumza na Uwazi kuhusiana na kifo hicho alisema wameshituka sana kwani kimetokea ghafla na marehemu alikuwa haumwi.
“Siku hiyo ya Jumatatu marehemu hakuonekana shuleni asubuhi jambo ambalo siyo kawaida yake kwani hakutoa taarifa ya kutofika, mazingira hayo yalimfanya mwalimu wa taaluma Donard Otiato kumpigia simu ambazo zilikuwa zinaita bila kupokelewa.
“Ilipofika jioni baadhi ya walimu wenzake walilazimika kwenda nyumbani kwake Kimara Baruti na walipofika waligonga mlango bila kuitikiwa, mmoja wao aliusukuma wakaingia ndani na kumkuta amelala kitandani.
“Walimuita lakini hakuitika, walipomuangalia vizuri waligundua kuwa amefariki dunia huku damu zikimtoka mdomoni, puani na ulimi ulikuwa umetoka nje. Pia alikuwa na alama za michubuko shingoni na sehemu nyingine za mwili huku vyombo vya ndani vikiwa vimevurugika.
“Ilivyoonekana kulikuwa na mapambano kati ya marehemu na muuaji. Walimu hao walinipigia simu na kunifahamisha walichokikuta, nikawaelekeza waite polisi au watoe taarifa.
 “Nilitoka kuelekea eneo la tukio, nikawakuta polisi wameshafika na walikuwa wanaendelea kuchukua maelezo kwa baadhi ya wananchi wa eneo hilo.
 “Kwa kweli tumempoteza mtu muhimu sana kwa shule yetu kwani marehemu alikuwa ni mchapakazi na mwenye ushirikiano mzuri kwa wenzake,” alisema mwalimu huyo.
Mwili wa Elizabeth uliagwa kwenye Shule ya Atlas huko Madale, Wilaya ya Kinondoni Jumatano ya wiki iliyopita na ukasafirishwa kupelekwa Karatu mkoani Arusha kwa mazishi.
Kilichoongeza simanzi ni wakati wa zoezi la kuuaga mwili wa marehemu ambapo baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo walilia hadi kufikia hatua ya kuzimia.
Aidha, kiongozi wa dini aliyekuwa akiendesha ibada ya mazishi aliyefahamika kwa jina la Mchungaji Leonard alisema muuaji wa mwalimu huyo atahukumiwa na Mungu kwani alichokifanya ni kitu kibaya sana.

Post a Comment

 
Top