Kituo kipya kilichofunguliwa cha Operesheni za Polisi Kenya, ambacho dhamira yake ni kuratibu na kutekeleza operesheni za kupambana na ugaidi pamoja na idara kadhaa za usalama wa taifa, kitaifanya Kenya na kanda nzima kuwa salama zaidi katika kukabiliana na vitisho vya wenye msimamo mkali, maafisa wasema.



Maafisa wa polisi wakiwa na mbwa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji katika kitongoji cha Eastleigh mjini Nairobi hapo tarehe 19 Novemba, 2012, siku moja baada ya bomu kulipuka katika basi dogo, na kuua watu saba. [Na Carl de Souza/AFP]


Kituo hicho kipya cha Nairobi kinachukua nafasi ya Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi chenye umri wa miaka 10, na ni hatua kubwa zaidi ukilinganisha na mtangulizi wake, alisema Boniface Mwaniki, mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU).


Kituo kimo katika jengo kubwa zaidi, ambacho kina teknolojia ya kisasa kabisa ya kusimamia operesheni za ufuatiliaji na uchunguzi. Kituo kina kompyuta mpya, mifumo ya kisasa ya mawasiliano, vitambuzi na vifaa vya kutegua milipuko, kwa mujibu wa maafisa.


"Kama unavyojua, huwezi kutarajia matokeo tofauti kwa kufanya vitu hivyo hivyo kila siku," Mwaniki aliiambia Sabahi. "Wanamgambo wamebadilisha mbinu juu ya jinsi ya kufanya mashambulizi na wamekuwa wa kisasa zaidi. Kwa hivyo, kwa kituo hiki tunajiweka mbele ya mchezo ili kuzima vizuri mipango yao mapema."


Kabla ya kituo kufunguliwa rasmi, serikali ilikitumia kituo hicho kufuatilia shughuli zinazoshukiwa wakati wa kampeni za uchaguzi na kuwasaidia maafisa wa polisi walioko kazini kupokea na kufanyia kazi ripoti za kikachero kutoka sehemu zinazojulikana kwa vurugu, alisema.



"Tuliweza kupeleka polisi mapema ili kusimamia sheria na kanuni, kitu kilichochangia sana kufanyika kwa uchaguzi wa amani," Mwaniki alisema.


Kikosi cha ufanisi zaidi kwa kupambana na ugaidi
Kituo kitafanya iwe rahisi zaidi kwa vyombo vya usalama kugawana habari na kuratibu juhudi zao na amri moja, alisema Oriri Onyango, mkuu wa Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Uhalifu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Umma nchini Kenya.


Hata baada ya mwaka 2003, wakati Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi kilipoanzishwa, ilikuwa vigumu kupata data za shughuli za kigaidi, Onyango alisema. Sasa, kituo hicho kipya kitasaidia rekodi za vyombo wa uimarishaji wa sheria, kuorodhesha na kugawana taarifa za usalama na ushahidi katika kesi zinazohusiana ambazo zinachunguzwa.


"Kuhifadhi vitu vya ushahidi pamoja na maandalizi ya ushahidi utakaotumika katika kuendesha mashitaka ya watuhumiwa wa ugaidi kumekuwa changamoto, lakini sasa kituo hicho kitakuwa kikishughulikia kwa umadhubuti zaidi uhalifu unaohusiana na ugaidi," alisema, na kuongeza kwamba serikali inadhamiria kukitumia kituo kwa kuwapa mafunzo maafisa katika kukabiliana na ugaidi.


Kituo hicho kitapaswa pia kupunguza makosa ya kipolisi, ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa kushindwa na mbinu katika vita dhidi ya ugaidi, alisema Simiyu Werunga, kepteni wa jeshi mstaafu na mshauri wa masuala ya usalama aliye na makao mjini Nairobi.


"Polisi wamekuwa [wakitegemea] na kazi za kufikiria tu linapokuja suala la kupambana na ugaidi," alisema. "Daima wamekuwa wakifanya kazi baada ya mlipuko kutokea, lakini kwa kituo kama hiki sasa wataweza kufanya kazi zaidi, jambo ambalo litasaidia kuzuia mashambulizi zaidi nchini Kenya."


Werunga, ambaye pia anaendesha Kituo cha Afrika cha Masomo ya Usalama na Mikakati, alisema kuwa ATPU kinapaswa kuendelea kuwapa mafunzo maafisa wake ili waweze kujiweka sawa na mwenendo wa mabadiliko katika ugaidi.


Msitari wa mbele wa vita dhidi ya ugaidi


Uingereza, ambayo iligharamia ujenzi wa kituo na vifaa, ilisema kuwa inadhamiria kusaidia juhudi za Kenya za kuzuia na kutokomeza vitisho vya ugaidi.


"Msaada wa Uingereza kwa kituo hiki ni ishara zaidi za dhamira iliyonayo Uingereza ya kufanya kazi na Kenya," Balozi wa Uingereza mjini Nairobi Christian Turner alisema wakati wa sherehe za ufunguzi hapo tarehe 2 Mei. "Kituo hiki kitasaidia nchi zetu kuendeleza ushirikiano wetu na kupambana na ugaidi."


Mwaka jana, katika kuisadia Kenya kupanua na kuimarisha kazi za polisi, Uingereza ilitoa msaada wa boti ya kujaza upepo kwa polisi wa Lamu, kifaa cha x-ray kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nairobi na kifaa cha ufuatiliaji wa operesheni za kupambana na uharamia.


Kwa vile sasa kimefunguliwa, Kituo cha Operesheni za Polisi Kenya kitakuwa katika mstari wambele katika vita vya nchi vya kupambana na ugaidi, kusaidia kuongeza ukusanyaji wa taarifa za kikachero na kufuatilia mienendo na shughuli za wanamgambo wanoshukiwa au watu wengine wenye misimamo mikali, Mwaniki alisema.


"Tutakuwa na uwezo wa kufuatilia shughulia za kigaidi za kikundi, na kufuatilia na kugundua milipuko kwa kutumia mashine tulizonazo hapa, kwa hivo tutaweza kuzuwia mashambulizi na kuwatia mbaroni washukiwa kabla ya kurusha mabomu yao," alisema.


Chanzo: sabahionline.com

Post a Comment

 
Top