http://www.immigration.go.tz/immigrt12.jpg
 
 
 
 
 
 
 
 
NAIBU Kamishna wa Uhamiaji, ambaye ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma,  Norah Massawe  amesema jumla ya Wahamiaji haramu 38 walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma kuanzia kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Katika mahojiano ofisini kwake na waandishi wa habari amesema  kati ya waliokamatwa wahamiaji wanne walihukumiwa vifungo kati ya miezi sita na mwaka moja.

Pia amebainisha kuwa, wahamiaji 34 walitozwa faini na kurudishwa nchini kwao na kati ya hao watano walikuwa ni wanawake na wanaume wakiwa na 33.

Naibu Kamishna huyo amezitaja nchi wanazotoka ni Kenya, Zambia, Afrika Kusini,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo na China na walipohojiwa walisema walikuja kutafuta ajira Tanzania  kwenye kazi mbalimbali kama muziki, saluni na hata uuzaji wa bidhaa.

Amesema sasa kumekuwa na mwamko mkubwa kwa  wananchi juu ya kuwatambua wahamiaji haramu na kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo husika kutokana na elimu inayoendelea kutolewa kuanzia ngazi za juu hadi kwenye vitongoji .

Norah amesema Idara ya Uhamiaji  inajipanga katika mikakati yake kukaa kwenye vizuizi vya barabarani ili kuwabaini wahamiaji wanaosafirishwa kwa kutumia mabasi, malori na njia nyingine.

Aidha amewataka wananchi kukubali kushirikiana na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dodoma ili kulinda amani na kuwa wazi bila kuogopa kutoa taarifa.

Amesema kuwa vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa kwa kutoa elimu na kuelimisha wananchi ambao wametambua athari za kukaa na watu wasiowatambua katika maeneo yao.

Post a Comment

 
Top