Stori:  Mwandishi Wetu, Mbeya
NDUGU wa marehemu Kassim Saidi Mboya (36) aliyekutwa na kete 65 za dawa za kulevya wilayani Kyela, mkoani Mbeya wiki iliyopita wako katika mashaka makubwa baada ya polisi mkoani hapa kusema watasakwa ili kujua zaidi juu ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Diwani Athumani amesema mwishoni mwa wiki kuwa ndugu hao wa Mboya ni lazima wasakwe ili waweze kuichukua maiti ya ndugu yao lakini pia kujua juu ya kile kilichokutwa ndani ya tumbo la marehemu.
“Wengi hivi sasa watakuwa matumbo moto maana polisi wanaweza kuwashikilia kwa ajili ya kuwahoji kama wana fununu na biashara ya madawa ya kulevya aliyokutwa nayo marehemu na wataisaidia polisi kujua marafiki wa karibu wa marehemu Mboya,” alisema polisi mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa polisi.
Kamanda Athumani alisema inaweza kuwa rahisi kuwapata ndugu wa marehemu kwa sababu maiti ya Mboya ilipokaguliwa ilikutwa na simu ya kiganjani ambayo itasaidia kuwapata watu wa karibu wa marehemu huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, marehemu alizidiwa alipokuwa anasafiri kwenda Malawi kwa basi lenye namba za usajili T.319 BLZ aina ya Nissan.
Alisema hata jina lililokutwa kwenye tiketi yake ya kusafiria lina utata kwani limeandikwa Kassim Mueck Michael, jina ambalo ni tofauti na lililokuwa kwenye hati ya kusafiria inayosomeka Kassim Said Mboya.
Amewataka wananchi kuachana na biashara haramu ya madawa ya kulevya na akatoa wito kwa wanayemfahamu marehemu Mboya kwenda kuitambua maiti yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Post a Comment

 
Top