Bank Ki Moon


Wagombea wa urais wa Zanzibar wa vyama sita, wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN), Ban Ki Moon kumwomba asaidie kutatua mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Vyama hivyo ni Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Chaumma, Sau, DP na NRA ambavyo mbali na kumweleza Ban kwamba hawakuridhishwa na kufutwa kwa matokeo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, pia wamemwomba aingilie kati mkwamo huo.

Katika barua hiyo, vyama hivyo vimesema vimevunjwa moyo na Jecha kufuta matokeo, wakati alitakiwa aendelee na kumtangaza mshindi ili kuepusha machafuko.

Mgombea wa NRA, Seif Ali Iddi alisema wameamua kuandika barua hiyo wakiamini kuwa UN inaweza kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Katibu mkuu wa Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir alisema wamepeleka barua UN kwa sababu hawana imani na Mwenyekiti wa ZEC na hawatambui uamuzi wake kwa kuwa hakukuwa na malalamiko.

Katibu Mkuu wa Chaumma, Ali Omar Juma: “Tunataka matokeo ya Zanzibar yatangazwe, pia tunataka mgogoro huu umalizwe na Jumuiya ya Mataifa iingilie kati na tunaomba kamati ya wataalamu kuchunguza na kupata ushahidi wa uchaguzi wa Zanzibar ulivyokwenda.”

Juma alithibitisha kumwandikia barua Ban iliyotiwa saini na wagombea hao sita wakitaka kuona mgogoro huo unatatuliwa kwa njia za kidiplomasia kwa kuwa wanaamini Serikali ya Tanzania haina nia ya kuutatua.

Vyama hivyo vimemweleza Ban kwamba, uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki na baadhi ya majimbo yalishatangazwa huku waangalizi wa ndani na wa kimataifa wakishuhudia lakini jambo la kusikitisha matokeo yasitishwa.

“Makamu mwenyekiti wakati anatangaza matokeo alisitishwa asiendelee huku tukasikia kupitia televisheni kwamba matokeo yamefutwa na Mwenyekiti Jecha. Sasa tunajiuliza, ni kwa nini yafutwe na mamlaka hayo ya kuyafuta kayatoa wapi?” alihoji Juma.

Barua hiyo iliyopokewa na ofisa wa UN, Alvaro Rodriguez ilisema jambo la kushangaza katika kufutwa kwa matokeo hayo ni kwamba hakuna malalamiko yaliowasilishwa na chama chochote cha siasa ambayo yangeweza kuonyesha kasoro za uchaguzi huo ilhali waangalizi wa ndani na nje wote waliona uchaguzi umekwenda kwa salama, amani na haki.

Wagombea hao walisema Umoja wa Mataifa ndiyo taasisi pekee inayoweza kutatua mgogoro huu na si Serikali ya Tanzania kwa madai kuwa tayari imeshavunja Katiba ya nchi kwa kushindwa kusimamia suala zima la hali iliyojitokeza Zanzibar. “...Inajua kwamba mwenyekiti hana mamlaka lakini kwa sababu ni mtu wao wanamwachia tu.”

Tangu kufutwa kwa matokeo Novemba 28 na Jecha, hali ya kisiasa Zanzibar bado haijatulia huku wananchi wakiwa na hofu ya kutokea kwa vurugu licha ya wanasiasa kuwatuliza wafuasi wao kila mara.

Post a Comment

 
Top