Vigogo TRA Wakutwa na Mamilioni Nyumbani Kwao
Siku chache baada ya kigogo mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubainika kumiliki nyumba 73, wafanyakazi wengine wa mamlaka hiyo wamekutwa na mamilioni ya shilingi waliyoficha majumbani mwao.


Taarifa kutoka ndani ya TRA zinapasha kuwa tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasimamishe kazi maofisa kadhaa wa mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kitengo cha uchunguzi cha mamlaka hiyo, hivi sasa wapo kwenye msako wa kubaini ukwasi wa wafanyakazi wake.


Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, juzi maofisa wa kitengo cha uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walifika katika eneo la Tegeta Salasala wilayani Kinondoni na kuvamia nyumba mbili za wafanyakazi wa mamlaka hiyo.


Katika nyumba hizo, wafanyakazi hao kila mmoja alikutwa na kiasi kikubwa cha fedha ndani kuliko kiwango cha mshahara anaolipwa.


“Walivamiwa wafanyakazi wawili (majina yanahifadhiwa), ambapo katika kila nyumba zilikutwa fedha nyingi. Kwa mtu wa kwanza zilikutwa Sh milioni 200 na yule wa jirani yake pia alikuwa na zaidi ya shilingi milioni 150.


“Tangu kuanza kwa msako huu wafanyakazi wengi wamekuwa hawana amani kabisa, na hata wengine wanasema wazi kama wangekuwa na uwekezaji wa nje ya nchi wangeondoka kabisa nchini,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.


Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wafanyakazi hivi sasa wamelazimika kuzikimbia nyumba zao na kuishia kulala hotelini huku wakienda kazini wakiwa na hofu.


Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa Kamishna wa Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki, aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo wengine wa mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa kontena 349 zenye thamani ya Sh bilioni 80, amebainika kumiliki nyumba 73.

Post a Comment

 
Top