NI zaidi ya ukatili! Katika hali isiyowahi kufikiriwa na binadamu aliyeumbwa na Mungu, baadhi ya vijana wa  Kijiji cha Mkwajuni Wilaya ya Chunya, Mbeya wamemzika akiwa hai aliyekuwa msaidizi wa padri, Katekista Flavian Mwamosi Mwachirui (68) wakimtuhumu kusababisha kifo cha Peter Robert (28) mkazi wa kijijini hapo.

Jeneza la marehemu Peter Robert baada ya kufukuliwa.
Tukio hilo lililoshtua wengi katika eneo hilo lilitokea saa nane mchana wa Ijumaa iliyopita kwenye Makaburi ya Maweni kufuatia kijana Peter kufariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mwili wa marehemu Mwamosi Mwachirui baada ya kufukuliwa.
DHAMBI ILIPOANZIA
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni ndugu wa mzee huyo (jina tunalo) aliweka wazi kwamba, dhambi ya ukatili huo wa kutisha ilianza pale marehemu Peter alipokumbwa na mauti akiwa anatibiwa kwa mganga wa kienyeji ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Simulizi hii ya kweli inaendelea kuwa, wakati ndugu na jamaa wakilia na kuomboleza na ratiba ya maziko ikitangazwa, ndipo baadhi ya ndugu hao wa marehemu waliibuka na kudai eti kifo cha Peter si cha Mungu, kwa sababu kilikuwa na mkono wa binadamu!
Dada wa marehemu Peter wakilia kwa uchungu.
NDUGU WAMWANIKA ‘MUUAJI’ WAO
Ndugu hao walipoona watu hawawaelewi waliposema marehemu kafa kwa kurogwa, wakaenda mbele zaidi, wakamtaja mzee Flavian Mwamosi Mwachirui ambaye ni katekista mstaafu aliyekuwa akihudumu katika Kigango cha Mkwajuni hadi 2007.

SIKU YA MAZISHI YAFIKA
Madai ya baadhi ya ndugu hao yalinaswa na vijana kadhaa wa kijiji hicho ambao waliapa kwa miungu wao kwamba lazima marehemu wamzike na ‘muuaji’ wake, yaani mzee Mwachirui. Inauma sana!
“Siku ya kumzika Peter, kuna vijana walisikika wakisema marehemu watamzika na mzee Mwachirui tena wakaongeza kuwa  watamzika mzee huyo akiwa hai ili aone maumivu ya kifo utadhani walimuona akimuua huyo Peter,” kilisema chanzo huku kikibubujika machozi.
Chanzo kikaongeza: “Watu wa huku wanaishi kwa kutumia akili za waganga wa kienyeji. Mganga akisema unakosa mazao shamba kwa sababu mama yako anakuroga, basi mama huyo atauawa! Mbeya si sehemu salama tena.”
Mwili wa mzee Mwachirui ukufukuliwa.
‘MUUAJI’ AITWA KUCHUNGULIA KABURI LAKE
Kaburi la kumzikia marehemu Peter lilimalizika kuchimbwa, vijana waliokuwa wakiliandaa waliagiza wazee wa kimila wafike kwa lengo la kuangalia utaratibu wa mazishi na kukagua ukubwa wa kaburi lenyewe kama lipo sawa.
Wito huo uliwagusa wazee wanne wa kijiji hicho, (masikini ya Mungu) akiwemo Mzee Mwachirui ambaye vijana hao walimsisitiza yeye asogee jirani kabisa na kaburi.
Bila kujua alibakiza sukunde chache za kuishi duniani, mzee huyo alisogea na kuchungulia kaburi ili atoe utafiti wake kwa vijana hao wenye moyo wa kikatili kuliko wanyama wa porini, akiwemo simba anayekula wenzake.
Kushoto ni mwili wa mzee Mwachirui baada ya kufukuliwa , kulia ni kaburi la Peter.
SAA YA KIFO INAFIKA
Ilikuwa kufumba na kufumbua, kijana mmoja aliyeshika sururu alimpiga nayo kichwani mzee huyo hali iliyomfanya ayumbe.
Kama vile haitoshi, wapo vijana waliomsindikiza kwa kumpiga na marungu hadi akaangukia kaburini.

MAISHA NDANI YA KABURI
Chanzo kikasema: Masikini mzee wa watu, alijaribu kujiokoa kwa kutaka kutoka kaburini lakini wale vijana wakamwamuru akae, alipokataa alizidi kupigwa.
“Ilifika mahali aliishiwa nguvu huku akijiona. Mbaya zaidi vijana waliokuwa wakimfanyia unyama huo anawajua kwa majina na alijaribu kuwaita mmoja mmoja ili wamwachie lakini wapi!”
Kinachoumiza zaidi, mzee huyo aliingia kaburini na nguo zake, suruali iliyofungwa mkanda mweusi, nguo ya ndani, shati jeupe la mikono mirefu lenye mistari ndani akiwa ametinga ‘singlendi’. Miguuni alikuwa pekuwa.

APOTEZA FAHAMU, WAMWEKEA JENEZA JUU YAKE, WATIA UDONGO
‘Wauaji’ hao walipojiridhisha kwamba mzee huyo hakuwa na uwezo wa kutoka kaburini, walichukua fito wakamfunika nazo kisha wakafukia udongo mchache, juu yake wakaliweka jeneza la marehemu Peter, wakafukia udongo kwa majembe na masepetu mpaka kaburi kukamilika. Ni zaidi ya ukatili uliowahi kufanywa mwaka 2013!

KAMA VILE HAITOSHI
Baada ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi la vijana lilipiga mbio hadi  nyumbani kwa marehemu mzee Mwachirui na kuiteketeza nyumba yake huku wakiapa kuwa, hakuna kutoa siri ya tukio hilo. Walisema walichokifanya ni ‘siri ya jeshi’.

WANAKIJIJI WAKERWA, WAKIMBILIA SERIKALINI
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walikimbia hadi kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Credo Kayanza na kumpa ripoti ya unyama huo.
Naye mwenyekiti alipoona ni unyama uliopita kiwango cha ubinadamu alishika njia hadi kwa diwani wa kata hiyo, Chesco Ngairo ambapo wote kwa pamoja walikimbia hadi Kituo cha Polisi Mkwajuni na kusema yote huku wakiomba maafande wenye uwezo wa kivita kufika kijijini hapo kushughulikia hali hiyo.

KABURI LAFUKULIWA
Polisi walifika kijijini hapo kwa spidi ya ndege ya kijeshi na kukuta tukio likiwa bichi, wakawaamuru baadhi ya vijana kulifukua kaburi hilo zoezi ambalo lilifanyika baada ya vijana hao kulipwa fedha!
Baada ya kufukua kaburi,
jeneza la marehemu Peter ndilo lililoanza kutolewa na kuwekwa pembeni, zikafuata fito kisha mwili wa marehmu mzee Mwachirui ambao uliwekwa pembeni pia.
Polisi wakaamuru mwili wa Peter uzikwe, wao wakaondoka na mwili wa mzee Mwachirui hadi Hospitali ya Misheni ya Mkwajuni kwa ajili ya uchunguzi na kujiridhisha juu ya kifo chake.
Madaktari waliokuwa zamu walithibitisha kuwa, mzee huyo alishaaga dunia, hivyo ndugu wakakabidhiwa mwili huo kwa ajili ya
kwenda kuuzika sehemu nyingine lakini katika makaburi alikozikwa Peter.

HUYU HAPA KAMANDA WA POLISI MBEYA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Diwani Athuman amethibitisha kutokea kwa tukio hilo,  pia ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia  ya kuamini mambo ya ushirikina na uchawi kwa madai kuwa hakuna faida zaidi ya kuchochea migogoro.

MADAI YA NYUMA
Kwa miaka mingi, marehemu mzee Mwachirui na wenzake wawili ambao majina yao hayakutajwa walikuwa wakituhumiwa kwa vitendo vya kishirikina licha ya kwamba hakuna aliyewahi kuona matukio yao laivu au kuwa na ushahidi mkononi.

Post a Comment

 
Top