TUKIO la kuuawa kwa mfanyabiashara kijana mwenye mafanikio, Ayoub Mlay, siyo tu linaacha simanzi kwa Watanzania bali pia ni fundisho kwa jamii na serikali.
Mwili wa marehemu Ayoub Mlay baada ya kupigwa risasi.
MLAY, alifariki dunia usiku wa Alhamisi iliyopita, Mei 16, mwaka huu baada ya kupigwa risasi kwenye Klabu ya Ambrosia, iliyopo Kawe Beach jijini Dar es Salaam.
Simanzi inakuja kwa sababu Mlay, 38, alikuwa mfanyabiashara kijana aliyeonesha mafanikio na kupiga hatua kubwa, amefikwa na mauti akiwa bado na moto wa kusaka maendeleo zaidi kwenye biashara zake na maisha kwa jumla.
Kwa Conrad ambaye ni kijana mdogo pia, anaingia kwenye msukosuko lakini nyuma yake kuna funzo la umiliki na matumizi sahihi ya silaha za moto ambazo kwa sasa zimekuwa kama ‘fasheni’ kwa vijana wengi wa mjini.

WOTE NI WATOTO WA ARUSHA
Mlay ni mfanyabiashara wa Arusha ingawa mara kwa mara hupatikana Dar es Salaam kutokana na mizunguko yake ya kibiashara.
Conrad, naye ni mwenyeji wa Arusha, ingawa kwa sasa makazi yake yapo Dar es Salaam.
Kuhusu kazi ya Conrad, mmoja wa watu waliohojiwa na gazeti hili nje ya Klabu ya Ambrosia, alisema: “Kwa kweli huwa tunamuona, wengi tunamuona ni mtoto wa mjini tu, kwani hatujui anajishughulisha na nini.”
Marehemu Mlay enzi za uhai wake.
CHANZO CHA UGOMVI
Mtoa habari wetu aliyeomba hifadhi ya jina lake gazetini, alisema kuwa Mlay na Conrad ni watu waliokuwa wanafahamiana na kuna jambo walikuwa wanazungumza.
“Siyo rahisi sana kujua walichokuwa wakizungumza ila baadaye yalitokea mabishano. Walitaka mpaka kushikana ili kupigana, watu wakawazuia. Inaonekana Conrad hakukubali, maana aliamua kutoka nje mbio.
“Kwa haraka haikujulikana alifuata nini kule nje, tuliokuwepo tuliamini ameamua kukimbia lakini kumbe alikuwa amefuata bastola. Aliporudi, alikuwa na bastola mkononi, baada ya hapo hata hakutaka kuzungumza maneno mengi, alimpiga Mlay risasi kisha akataka kutoweka,” kilisema chanzo chetu.

WALINZI WALIVYOMDAKA
Chanzo chetu kilibainisha kuwa wakati anapita na bastola kuingia ndani, walinzi walimpisha kwa sababu ya kuhofia usalama wao lakini kipindi cha kutoka, walijipanga kumdhibiti.
Kiliendelea kusema, Conrad akiwa anatoka, walinzi walifanya kama wanampisha na baada ya kupita, walimbana mikono na kumnyang’anya bastola kisha wakamfunga kamba kabla ya kupiga simu kuita polisi.
Dakika kadhaa baada ya kupiga simu, polisi walifika na kufanya mahojiano na watu waliokuwepo eneo la tukio, kabla ya kumchukua mtuhumiwa na kumpeleka Kituo cha Polisi Kawe, Dar es Salaam.
Vilevile, polisi walimchukua Mlay na kumuwahisha Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu, Kinondoni, Dar es Salaam ili akapatiwe matibabu lakini baadaye ilibainika alikuwa ameshakata roho.
ACP Charles Kenyela.
MADAI KUHUSU MATUMIZI MABAYA YA SILAHA
Kwa mujibu mtu aliyejitambulisha kwa jina la Matidau, Conrad alikuwa na mazoea ya muda mrefu ya kuonesha bastola yake na kuwatishia watu aliotofautiana nao.
“Tunamjua Conrad, kuna watu walishamwonya lakini hakusikia, ikafikia wakati kwamba anapoanza ugomvi, basi tunaomjua tunakaa mbali naye kwa sababu lolote linaweza kutokea.
“Kuna kipindi alinyang’anywa bastola kwa sababu ya tabia yake ya kuioneshaonesha ovyo pamoja na kutishia watu. Tukio hili la mauaji ya Mlay linatufanya tujiulize hiyo bastola alirejeshewa katika mazingira gani au ni nyingine?” kilihoji chanzo.

MINONG’ONO KUHUSU FEDHA
Kuhusu kile ambacho Mlay na Conrad walibishana, kulikuwa na maneno ya pembeni kutoka wa watu waliokuwepo eneo la tukio kwamba chanzo cha ugomvi ni fedha.
“Unajua inapotokea matukio makubwa kama haya, watu wa eneo la tukio wakati mwingine ndiyo huwa wa kwanza kupotosha. Kwa mfano, yapo madai kuwa Mlay alimtuma kazi Conrad, sasa baadaye kukawa na mabishano kuhusu malipo.
“Yote yatazungumzwa lakini jambo ni baya sana. Fikiria kwamba Mlay ni mtu aliyekuwa ameajiri watu, ana familia na marafiki, wote hao wataathirika kwa namna moja au nyingine kwa kumpoteza mtu waliyempenda,” alisema mtoa habari wetu.
Mlay enzi za uhai wake.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Charles Kenyela alisema kuwa ni kweli tukio hilo lilitokea na akaongeza kuwa Conrad alimfyatulia Mlay risasi ya kifua.
Kuhusu madai kwamba Conrad ni mzoeafu wa tabia za kuchezea silaha na kutisha watu kiasi kwamba hata jeshi lake lina taarifa na liliwahi kumnyang’anya kabla ya kumrudishia kinyemela, Kenyela alijibu: “Hizo taarifa sina, ngoja nizifuatilie kwanza, maana siwezi kuzungumza jambo nisilo na uhakika nalo.
“Nilicho na uhakika nacho ni hiki; kwamba mtuhumiwa tunamshikilia na tutamfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.”

KIFUATACHO
Bado kuna maswali kuhusu tukio hili, timu nzima ya Kampeni ya Fichua Maovu ya Global Publishers, imejipanga sawasawa kufuatilia kwa kina na mara itakapokamilika, mambo yatakuwa hadharani kupitia magazeti yake ambayo ni damu moja na hili; Risasi, Amani, Ijumaa na Ijumaa Wikienda.
CHANZO : GPL

Post a Comment

 
Top