Na Waandishi Wetu
KIJANA mmoja mkazi wa Kurasini jijini Dar, Francis Huruma maarufu kwa jina la Big anayedaiwa kuuza madawa ya kulevya aina ya bangi, amemchinja polisi mwenye namba H.617 Anthony Pasco (22).
Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Ugimbi uliopo Kurasini, Dar.
Mbali na kumchinja kwa kisu polisi huyo shingoni na kutofanikiwa kumuua kama alivyokusudia, Big pia alimjeruhi vibaya polisi mwingine mwenye namba H.334 Akili Mlawa (23) kwa kisu mguuni na mkononi.
Polisi wote waliopatwa na majeraha wamelazwa katika Hospitali ya Jeshi la Polisi, Kilwa Road, jijini Dar.
Raia walioshuhudia tukio hilo, walimvamia Big kisha wakamshushia kipigo na baadaye akafariki dunia wakati akitibiwa katika Hospitali ya Temeke, Dar.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Engelbert Kiondo alisema kuwa Big alifariki dunia katika hospitali hiyo wakati akipatiwa matibabu ya majeraha yaliyosababishwa na kipigo.
Awali, wakazi wa eneo hilo walitoa taarifa polisi kutokana na kijana huyo kudaiwa kuendeleza uuzaji wa madawa ya kulevya na pombe aina ya viroba, jambo lililodaiwa kuchochea uhalifu katika kitongoji chao.
Ilidaiwa kuwa Big alikuwa akiwasababisha vijana wengi kutofanya kazi na kutumia muda mwingi kuvuta madawa ya kulevya kisha kufanya uhalifu eneo hilo.
Kamanda Kiondo alisema polisi walifanya msako mkali wa kupambana na uhalifu na kufanikiwa kumtia mbaroni kijana huyo.
“Big alikuwa mbogo na kufanikiwa kumchinja Pasco shingoni lakini hakufanikisha lengo lake la kutaka kumuua,” alisema Kamanda Kiondo.
Baada ya kuona Big amewashambulia polisi, wananchi waliongeza nguvu na kutoa msaada kwa kutumia matofali kumshushia kichapo kijana huyo.
Kamanda Kiondo alisema polisi wengine waliokuwa katika zoezi hilo, walimuokoa Big kutoka kwenye kichapo hicho na kumpakia kwenye gari kisha  kumkimbiza kituoni na baadaye katika  Hospitali ya Temeke.
Big alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Temeke ambako hakuna ndugu yake yeyote aliyejitokeza kwa ajili ya kumuwekea dhamana na baada ya kufanyiwa vipimo alionekana kuwa na malaria pamoja na maumivu makali kutokana na kipigo.
Jitihada za kuokoa maisha ya Big zilishindikana kwani alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu.
Hata hivyo, Kamanda Kiondo alisema msako mkali bado unaendelea katika Mkoa wa Kipolisi wa Temeke hasa maeneo ya Mtongani na Mto Mzinga ambako vijana wengi wanafanya uhalifu na kutumia muda mwingi kucheza kamari, kuvuta bangi na kulala na wake za watu kwa kuwatishia wenye wake zao.
“Wazazi wengi wamekuwa wakiwaficha vijana wao pindi wanapotafutwa kwa uhalifu kwani fedha wanazopata kwa njia hizo, nao huzitumia.
“Jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kupambana nao,” alisisitiza Kamanda Kiondo.
Polisi waliojeruhiwa wote wanaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Kilwa Road.
Imeripotiwa na Makongoro Oging’, Gladness Mallya na Issa Mnally
CHANZO :GPL

Post a Comment

 
Top