KAMPUNI ya simu za mkononi ya Tigo imezindua mtandao wa intaneti wenye kasi kubwa wa 4G unaokwenda mpaka spidi 42 Mbps.

Kwa kasi hiyo watumiaji wa Tigo sasa wataweza kuangalia video moja kwa moja kwenye mtandao bila kupakua kwanza, wanaweza kupakua kutoka katika mtandao kitu wanachokitaka na kukihifadhi, kupakia kitu katika mtandao na kucheza michezo mbalimbali ya kwenye mtandao.

Uzinduzi wa huduma hiyo ulifanywa kwa njia ya mkutano kupitia mfumo wa video wa Skype kwa kuunganisha mikoa minne huku hotuba hiyo ya uzinduzi ikisomwa na Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez kutoka makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Dar es Salaam.

Mikoa iliyoshiriki katika mkutano huo wa uzinduzi ni pamoja na Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Morogoro.

“Tunatambua haja ya wadau wetu, mabadiliko wanayotaka kila mara kwa ajili ya kuwatumikia vyema, tunatambua haja yao ya kuwa na mtandao bora wenye kasi inayokidhi mahitaji yao na mara zote sisi huwa tunawapatia bidhaa bora zinazokidhi mahitaji yao kwa bei rahisi. Bidhaa hii ni sehemu ya kuuboresha mtandao wetu,” alisema.

Meneja huyo alisema kwamba soko la mtandao kwa kutumia simu za viganjani limekuwa likikua na hivyo kuwa muhimu kwa watoaji mawasiliano ya simu kwani kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi mwaka 2012 kulikuwa na watumiaji milioni tano wa huduma hiyo.

"Kwa kuingiza katika soko huduma hii ya kasi ya ziada ya 42Mbps kunaonesha dhamira yetu ya kuwa mbele katika soko katika kutoa huduma bomba na yenye kuridhisha wateja,” alisema Gutierrez.

Aidha katika mkutano huo kwa njia ya video, waandishi wa habari walipata nafasi ya kuulizwa maswali ya papo kwa hapo na kujibiwa katika muda ambao ni wa kasi kabisa. Mkutano huo wa waandishi wa habari ulifuatiwa na mashindano ya michezo katika mtandao iliyoshirikisha vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Post a Comment

 
Top