KIONGOZI wa vijana wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) chake Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai amewekwa rumande siku saba baada ya kudaiwa kumuita Rais Robert Mugabe kuwa “punda anayechechemea.”
Kiongozi huyo Solomon Madzore aliyekamatwa mwishoni mwa wiki alipewa dhamana na hakimu alipofikishwa kortini Jumatatu mjini Bindura lakini dhamana hiyo ikapingwa na upande wa serikali.
Atakaa rumande siku saba. Katika kipindi hicho, upande wa mashtaka utakuwa na uhuru wa kukata rufaa uamuzi wa kumpa dhamana na $100 (Ksh 8,300).
Alidaiwa kumtusi Mugabe katika mkutano ulioandaliwa Aprili 27 ambapo alisema kiongozi huyo mkongwe ni “punda anayechechemea ambaye ameifanya vigumu kwa Tsvangirai kutawala vyema katika serikali ya muungano.”
Mwaka uliopita Madzore, alikaa rumande miezi kadha baada ya kudaiwa kumuua afisa wa polisi.
Shirika la kutetea haki la Zimbabwe Lawyers for Human Rights (ZLHR) limesema watu 60 wamekamatwa na kushtakiwa kwa kumtusi Mugabe katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Baadhi yao ni mawaziri wa chama cha MDC.
Post a Comment