MBUNGE wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amesema hana shaka na umaarufu wake Monduli wala Tanzania kwa ujumla.
 
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifungua kampeni za udiwani wa Kata ya Makuyuni huku akikishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupeleka mgombea wake katika Kata hiyo.

“Eti hawa wanathubutu kujinadi na kujigamba kushinda udiwani Monduli ya Lowassa wakisema watapata kura kwa asilimia 90 jamani haya ni kweli?,” alihoji Lowassa na kuongeza:

“Ndugu zangu sina shaka na umaarufu wangu Monduli wala Tanzania.”

Katika mkutano huo, aliwaambia wananchi kwamba anahitaji kuona wakikiadhibu CHADEMA kwa kukipa pigo ambalo hawajawahi kulipata mahali popote nchini.

“Ndugu zangu atakayewapa kura hawa CHADEMA wana wa Makuyuni atakuwa amenichoma kisu mimi, naomba msiwape kura hata moja, naomba muwafundishe adabu,” alisema Lowassa.

Akikishambulia chama hicho kwa kutumia helikopta katika Kata hiyo, alisema siku zote vita vya kiafrika vinapiganwa kwa kutumia askari wa miguu na si helikopita.

Alisema CCM inatumia askari wa miguu kuhakikisha inashinda vita vyake, hivyo haitatishika na helikopita hiyo.

Alikirushia kombora chama hicho kwa kukitaka kisimame hadharani na kujipapanua kama hakihusiki na vurugu zinazoendelea nchini.

Alisema kama kweli hakihusiki na vurugu zilizopo nchini basi viongozi hao wanapaswa kujihoji ndani ya nafsi zao kama kweli hawahusiki.

“Nawaomba hawa CHADEMA wajihoji ndani ya nafsi zao kama kweli hawahusiki na vurugu hizi, je wanaifanyia nchi yetu mema au mabaya,” alihoji Lowassa.

Post a Comment

 
Top