Rais Uhuru Kenyatta akisalimiana na Rais Barack Obama




RAIS Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa viongozi 47 wa Afrika walioalikwa na Rais wa Amerika Barack Obama kwa mkutano unaofanyika Washington DC Agosti mwaka huu.

Kulingana na taarifa ya msemaji wa White House, Bw John Carney, kiongozi huyo wa Amerika atawakaribisha viongozi hao wa Afrika katika juhudi za kupanua ushirikiano wa Amerika wa kibiashara, maendeleo na usalama katika bara ambalo linaendelea kupata mabadiliko na pia ambapo ana jamaa zake.

Mazungumzo hayo yatafanyika Agosti 5 na 6, ambapo kiongozi huyo atatimiza ahadi yake ya kufanya mkutano na viongozi wa Afrika. Alitoa ahadi hiyo katika ziara yake ya Afrika Juni mwaka jana. Bw Obama alitoa taarifa hiyo akiwa Cape Town, Afrika Kusini.

Obama anatarajiwa kukabili ushawishi mkubwa wa China barani Afrika.

Mwaliko wa mkutano huo utatumwa kwa mataifa yote ya Afrika ambayo yana uhusiano mzuri na Amerika na ambayo hayajasimamishwa kutoka kwa Muungano wa Afrika (AU).

Kenya ni miongoni mwa nchi kwenye orodha iliyosambazwa na White House hata ingawaje awali Amerika ilituma tahadhari kuwa itakuwa tu na mawasiliano ya muhimu na kiongozi wa Kenya kutokana na mashtaka dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kesi ya ICC

Septemba mwaka jana, Rais Kenyatta alitarajiwa kuongoza ujumbe wa Kenya kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York lakini ulifutiliwa mbali dakika ya mwisho kwa sababu Naibu Rais William Ruto hakuwa nchini wakati huo kwa kuwa alikuwa akihudhuria kesi yake katika ICC, The Hague, Uholanzi.

Rais Obama na Rais Kenyatta hata hivyo, wamezungumza kwa simu wakati kiongozi huyo wa Amerika alielezea kuwa pamoja na watu wa Kenya wakati wa shambulizi la kigaidi lililotokea katika jumba la kibiashara la Westgate.

Misri, Zimbabwe, Guinea Bissau na Madagascar ni miongoni mwa nchi ambazo hazijaalikwa.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir, ambaye pia anatakikana na mahakama hiyo ya ICC pia hataalikwa.

Post a Comment

 
Top