Mwanamuziki Muhidini Maalim Gurumo akiwa mahututi katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Stori: Oscar Ndauka
MWANAMUZI nguli wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Maalim Gurumo aliyefahamika pia kama kamanda na mashabiki wa muziki wa dansi, aliyeaga dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar, alikutana na mateso ya kwa saa 72 za mwisho wake baada ya kulazwa akiwa taabani kwa siku tatu.
Mtoto wa marehemu anayejulikana kwa jina la Abdalah aliliambia gazeti hili kuwa siku mauti yalipomfika baba yake katika wodi namba sita Jengo la Mwaisela, alimtembelea na kumkuta akiwa katika hali nzuri na alipopewa chakula alikula, akashiba lakini cha ajabu alisema hatakula tena.
Kijana huyo alisema muda mfupi baadaye, hali ya baba yake ilibadilika, akaanza kupumua kwa shida ndipo alipozidiwa na baadaye kukata roho.
Maalim Gurumo akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya kufikwa na mauti.
Mzee Gurumo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kwa muda mrefu na aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo ya Muhimbili.
Baadhi ya watu waliomtembelea mzee Gurumo kwa nyakati tofauti akiwa hospitalini hapo ni pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alimuombea afya njema na akaruhusiwa kurudi nyumbani.
Mzee Gurumo akiimba wakati wa uhai wake.
Kifo chake kimeacha simanzi si tu kwa familia yake, bali kwa wadau wa muziki wa dansi kwani alikuwa mwalimu na kiongozi wa wanamuziki wengi ambao sasa wanatamba. Baada ya kustaafu muziki, Mzee aliwahi kupewa zawadi ya gari na msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ aina ya Toyota Funcargo.
Akizungumzia msiba huo, Kiongozi wa Bendi ya Extra Bongo, Ally Choki alisema wamempoteza mwalimu wa muziki asiyekuwa na choyo ya kuelimisha.
Mzee Gurumo akiwa na mkewe.
“Ni kama tumepoteza tochi tukiwa kwenye msitu mnene usiku wa manane,” alisema.
Naye msemaji wa Bendi ya Mlimani Park Ochestra (Sikinde Ngoma ya Ukae), Jimmy Chika alipozungumza na gazeti hili alisema mzee Gurumo aliwahi kuja kuwatembelea na kuimba mwezi mmoja uliopita katika Ukumbi wa DDC, Kariakoo jijini Dar.
“Alikuja kama mara tatu hivi ukumbini, naona alikuwa kama anatuaga kwa sababu alikuwa mwanzilishi wa bendi na mbunifu wa mtindo wa Sikinde, aliubuni Septemba, 1978,” alisema Chika.Mzee Kassim Mapili, mwanamuziki wa mkongwe, kwa upande wake alisema kifo cha Gurumo ni pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibika na akafafanua kuwa ni mtu ambaye hakuwa mbinafsi.
Mzee Gurumo akiwa na CD yenye nyimbo zake.
Baadhi ya wanamuziki ambao amefanya nao kazi kwa karibu ambao sasa watakuwa wanamlilia mwalimu wao ni pamoja na Hassan Rehani Bitchuka, Said Mabela, Roman Mng’ande ‘Romario’ na wengine wengi.
Gurumo pia ameacha simanzi katika miji mbalimbali nchini kwa kuwa amewahi kutembelea kimuziki na alifanikiwa kujizolea mashabiki lukuki.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni msiba ulikuwa nyumbani kwake Mabibo, Dar huku taratibu za mazishi zikifanyika. Ameacha mjane na watoto wanne.
Mungu ailaze roho ya marehemu maali pema peponi. Amina.
-GPL
Post a Comment