Aliyejifanya Askari Polisi wa Usalama Barabarani, James Hassan (54) amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na sare za Polisi na kujifanya mtumishi wa jeshi hilo.

Aidha, adhabu hiyo ilitokana na makosa mawili ambapo mshitakiwa huyo atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu mitatu kwa kila kosa.
 
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema kwamba ametoa adhabu hiyo ambayo haitaenda kwa pamoja, kutokana na mshitakiwa huyo kuwa ni mkosefu mzoefu.
 
Pia alisema kwamba mahakama hiyo imemtia hatiani kupitia kwa mashahidi watatu wa upande wa mashitaka walioithibitishia mahakama bila ya kuacha shaka.
 
Kabla ya hukumu, mshitakiwa huyo alidai kwamba kwa kuwa mahakama imemwona kuwa ana hatia, yeye hakufanya kosa hilo na hata ikiwezekana mahakama imuachie huru.
 
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na badala yake alihukumiwa kifungo hicho.
 
Wakili wa serikali, Florida Wenuslaus alidai kuwa mshitakiwa apewe adhabu iwe fundisho kwa wengine.
 
Katika kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa, ilibainika kwamba mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, katika mahakama ya Wilaya ya Isanga, Dodoma na kufungwa katika gereza la Isanga mkoani humo.
 
Pia mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Polisi.
 
Katika barua iliyoandikwa na Mkuu wa Gereza la Keko kwenda kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, iliithibitishia mahakama kwamba mshitakiwa huyo alikuwa na kesi namba 32 ya mwaka 2004 na kwamba mshitakiwa alijiandikisha kwa jina la Ally Kinanda.
 
Pia barua hiyo ilieleza kuwa Hassan alitoroka akiwa chini ya uangalizi wa jeshi hilo na kwamba asipatiwe dhamana baada ya kukamatwa na kufikishwa katika mahakamana hiyo, kwa kuwa mshitakiwa alikana kuhusika na tuhuma hizo na kueleza kuwa watafuata taratibu zote kuchukua alama za vidole ili kuthibitisha kabla ya kupatiwa dhamana.
 
Ilidaiwa kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 14, 2014 maeneo ya Kinyerezi mnara wa Voda akijifanya kwamba ni askari polisi wa Usalama barabarani.

Post a Comment

 
Top