NI madai ya chini kwa chini kutoka vyanzo vilivyo karibu na mwanamuziki nyota nchini Uganda, Zarina Hassan ‘Zari The Bosslady’ ambaye kwa sasa ameshikamana kimapenzi na Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kwamba, utajiri anaoutangaza kuwa nao siyo kweli!
Mwanamuziki nyota nchini Uganda, Zarina Hassan ‘Zari The Bosslady’.
Madai hayo yalilishangaza Risasi Jumamosi kiasi cha kutaka kusikia kwa kina kwa nini utajiri huo siyo wa kweli wakati Zari anaonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa na mali zake, kama nyumba na magari?
MSIKIE HUYU
“Mimi ndiyo nawaambia. Zari kweli anajiwezaweza lakini si kwa mali anazozitangaza kuwa nazo. Mimi naishi Uganda, namjua vizuri sana Zari,” alisema mtoa habari huyo.
Risasi Jumamosi: “Twende polepole. Ina maana yale magari ambayo kwenye namba za usajili badala ya namba kumeandikwa ZARI GP, ZARI 3 GP, ZARI 1 GP, ZARI H GP na mengineyo mengi si ya kwake?”
Mtoa habari: “Mengine yake, mengine si yake.”
Risasi Jumamosi: “Kwa nini yawe si yake wakati yameandikwa Zari?”
Mtoa habari: “Kuna makampuni ya nje ambayo yakitoa magari yanaingia naye mkataba yeye ili kuyatangaza. Sasa kwenye mkataba Zari anatakiwa kubandika jina lake ili watu wajue staa mkubwa kama Zari naye anatumia magari kama yale.”
KUHUSU NYUMBA?
Mtoa habari huyo alisema anavyojua yeye, Zari ana nyumba moja nchini Uganda na nyingine Afrika Kusini ambazo aliachiwa na mumewe wa ndoa, Ivan Ssemwanga wakati wanatengana.
“Ile nyumba alijenga akiwa na mume wake, Ivan, lakini Zari kama Zari hajajenga. Hata sehemu kubwa ya mali zake Zari mumewe ndiyo amefanikisha.”
VIGEZO VYA MADAI
Mtoa habari wetu alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, kwa uhalisia wa magari ya Zari yanaweza kufika ishirini jambo ambalo alisema haoni mantiki yake.“Zari anasema anamiliki shule, vyuo, magari na mahoteli, lakini ili avipate hivyo maana yake amefanya biashara za kumzalishia, si ndiyo? Sasa kwa mfanyabiashara wa kweli anaweza kununua magari ya kutembelea ya kifahari kumi na tano na yuko yeye na watoto wake watatu tu? Tena wadogo.
“Tabia ya mtu kununua kila gari la kifahari linaloingia ni ya wale watoto ambao baba zao ndiyo wenye mali. Lakini kwa mfanyabiashara anayetunza mtaji wake, hawezi kununua kila toleo la gari.
“Kama itatokea hivyo, basi atauza lile gari la mwanzo na kununua jingine. Matajiri wote duniani wana magari ya kifahari ya saizi ya familia. Anaweza kuwa nayo mengi lakini matumizi pia ni hivyohivyo, sasa Zari magari kumi na tano halafu yeye na wanae watatu, wadogo. Mimi nakataa jamani,” alisema mtonyaji huyo.
KUJA KWAKE BONGO
Mtu huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, kama Zari anamiliki zile Hammer ambazo bei ya chini kabisa moja ni kama shilingi milioni mia mbili, basi hata kuja kwake Bongo kumfuata Diamond, angekuwa na utaratibu huu:
“Kwanza, kwa utajiri anaosema anao, mjue pesa ina tabia ya kusema. Zari angekuwa akitaka kuja Bongo kumfuata Diamond, angekuwa anatanguliza gari lake moja la kifahari likiwa na dereva ambalo angekuwa akilitumia nchini halafu yeye angekuwa anafuata na ndege. “Sasa yeye anakuja na ndege, akifika anategemea kutumia BMW C6 la Diamond. Sidhani kama kwa utajiri anaoutangaza anao angekuwa anafanya hivyo,” alisema mtu huyo.
TURUDI KWENYE MADAI YA ZARI
Katika mahojiano na Kipindi cha The Sporah Show cha mtangazaji Sporah Njau nchini Uingereza, Zari mwenye maskani yake Kampala na Afrika Kusini, alisema anamiliki ndinga kibao za kifahari zenye thamani kubwa.
MITANDAO YA UGANDA
Mitandao mbalimbali ya nchini Uganda, imebainisha kuwa Zari anamiliki BMW (2006) lenye thamani ya dola 47, 000 (Sh. milioni 75.2), Black Chrysler (2008) dola 16,000 (Sh. milioni 25.6) na Audi Q7 (2010) la dola 53,000 (Sh. milioni 84.8).
Mengine ni Silver Chrysler (2008) la dola 13,000 (Sh. milioni 20.8), Jetta Volkswagen (2006) linalomgharimu dola 27,000 (Sh. milioni 43.2), Mercedes Benz Convertible (2008) linalouzwa dola 26,000 (Sh. milioni 41.6) na Range Rover Sports (2010) lenye thamani ya dola 109,000 (Sh. milioni 174.4).
Pia ana Lamborghini Gallardo (2010) lililomgharimu dola 198,000 (Sh. milioni 316.8), Hummer H2 la dola 150,000 (Sh. milioni 240) na mengine mengi, yote yakiwa na jina lake badala ya namba za usajili.
KWENYE MAHOJIANO NA SPORAH
Zari alisema ana mjengo wa nguvu mjini Cape Town, Afrika Kusini na Apartments (nyumba za kupangisha na kila kitu ndani) jijini Kampala, Uganda.Jarida la Times la nchini Uganda linamtaja Zari kama mwanamke anayekaribia kuingia kwenye orodha ya wanawake matajiri Afrika.
DIAMOND ASHTUKA
Alipotafutwa Diamond na kuambiwa kwamba kuna habari utajiri wa Zari ni magumashi, alishtuka.
“Khaa zimetoka wapi hizo habari? Mbona mimi najua ni mali zake?” alisikika Diamond na kukata simu.
Jitihada za kumpata Zari ili aweze kuzungumzia utajiri wake hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani. Jitahada zinaendelea.
Chanzo: Gazeti Risasi via Gpl
Post a Comment