Mwandishi filamu za Jacob ‘JB’ Stephen, Daniel Manege amemtetea muigizaji huyo kuwa hakuwa na makosa ya kuigiza filamu ya ‘Mzee wa Swagga’ ambayo ni kopi ya filamu ya kihindi, Ladies Vs Ricky Bahl.

Manege aliyeiandika filamu hiyo pamoja na zingine zikiwemo Dereva Taxi, Nakwenda kwa Mwanangu, Shikamoo Mzee, Bado Natafuta zingine, ameandika ujumbe kupitia Facebook na kudai kuwa JB si mtu wa kulaumiwa bali ni yeye mwandishi.

“Kwanza kabisa ningeanza kwa salam kwenu nyote na naamini muwazima wa afya. Nimeamua kuandika ujumbe huu baada ya kuona na kupigiwa simu chache kuhusu uvumi wa filamu Mzee wa Swagga kuwa imekopiwa. Nijibu jibu fupi bila kusita kuwa kweli Story imekopiwa na original Story inaitwa Ladies Vs Ricky Bahl na mimi ndiye niliyemshauri JB kuichukua Story hiyo yenye maudhui ya kuvutia,” ameandika.

“Nataka nieleze sababu ya kufanya hivyo ila kabla sijaeleza sababu ningependa kuwaambia wale wote wanaotumia skendo hii kuyarefusha mambo haya kuwa kwenye ulimwengu wa filamu ni jambo la kawaida duniani watu kuchukua maudhui ya story na kuyatengeneza katika mazingira yao endapo maudhui hayo yataelimisha au kukosoa au kufurahisha kuhusu jambo..watakaoendelea kulalamika baada ya ujumbe huu ni dhahiri wanania zao nyingine na si kujenga.”

Kwanza kabisa mimi ndiye mwandishi mkubwa wa filamu za JB kuanzia enzi za DJ Ben, Dereva Taxi, Nakwenda kwa Mwanangu, Shikamoo Mzee, Bado Natafuta mpaka hii Mzee wa Swagga na hizo nyingine zote zikiwa ni original scripts kutoka kwenye ubongo wangu. Filamu anazofanya JB ni Romantic Comedies na Inspirational Comedies kwa hiyo yeye huwa anapenda maudhui ya kuentertain zaidi yani filamu zenye kuchangamsha na kuburudisha tofauti na waigizaji wengine kama Single Mtambalike anayependelea filamu za ugentleman zaidi (haya ni kutokana na kukaa nao na kuzungumza nao na kuwafahamu kwa kina)

Sasa kuhusu Mzee wa Swagga, JB alitengeneza filamu mfululizo zenye maudhui tofauti na alizozoeleka, kama Hukumu ya Ndoa, Mikono Salama ambazo sikuziandika mimi na nakiri kuwa hazikufanya vizuri sana sokoni. Sababu ya filamu hizi kuandikwa na watu wengine ni sababu nilikuwa nashughulika na Script ya filamu yangu mwenyewe niliyoproduce mwaka jana October inayoitwa SAFARI YA GWALU (bado haijatoka mpaka mwezi wa 3 mwishoni), aliyoigiza Gabo kama kijana anayerudi shule ya msingi baada ya kupigika na maisha.

Filamu hii imenichukua mwaka mzima kuanzia kuiandika mpaka kuja kuproduce, kuandika ilianza January-march 2014 hivyo sikupata nafasi kumuandikia JB tangu tulipotoa BADO NATAFUTA na CHARLE MVUVI (bado haijatoka). Baada ya filamu hizi mbili (Hukumu ya Ndoa na Mikono Salama) JB alinieleza angetamani nimuandalie Filamu na Mzee Majuto wakati huo wakiwa safarini kwenda Uturuki ili wakashoot Uturuki iwe filamu kali. Wakati nikiandaa filamu hiyo mshtuko mkubwa ukaja kwa misiba ya mfululizo ya wana Tasnia wenzetu iliyopelekea Safari ya JB na Mzee Majuto ya Uturuki kufa na hivyo kufanya hata script niliyoandaa kukosa msisimko tena.

Baada ya matatizo JB alitaka filamu inayofanana na Senior Bachelor, DJ Ben na Nakwenda kwa Mwanangu, akiigiza kama mburudishaji zaidi na kwa kuwa sikuwa na Idea mpya kwenye kichwa na muda ulikuwa unaenda sana na anahitajika kupeleka filamu yake kwa msambazaji ikabidi nitafute story itakayofanana na JB mburudishaji tunayemfahamu muda mrefu, kwa kuwa mimi ni gwiji wa filamu haikuwa ngumu kutafuta na ndipo tukaipata Ladies Vs Rick Bahl, JB aliipenda ila sote tulikuwa na wasiwasi kwani JB ni muoga sana wa kuandikwa vibaya, nikamwambia jambo ambalo nataka niwaeleze nanyi leo. Jambo ambalo lilimfanya JB kukubali niandike script mpya kupitia kisa kile na kuiproduce..

Ukweli ni kuwa duniani kote watu wanapoona maudhui ya story ya nchi au taifa jingine kuwavutia wanaweza kuchukua maudhui hayo na kuyatumia kutengeneza filamu za maudhui yale kwenye mazingira yao. Kuna Filamu nyingi hapa Tanzania na Nigeria na Bollywood Hata Hollywood zimefanyika hivyo na si dhambi. Kama Tanzania tazama filamu Ya BEST MAN ya Hemedi na Yussuf Mlela, ni copy ya BEST MAN ya Morris Chestnut na Taye Diggs… Nollywood filamu Ya GUARDIAN ANGEL ya Ramsey Noah ni copy ya Filamu HATYA ya Bollywood ya Govindah…Pia filamu za ROMEO AND JULIET developed kutoka kwa William Shakespears plays zimekopiwa Bollywood kwenye filamu iliyoleta Mabadiliko makubwa Bollywood ya QAYAMAT SE QAYAMAT TAK kama nasema uongo mtu aziangalie na kuja kunikosoa na nitaleta dazeni ya filamu zilizokopiwa kutoka nchi na nchi. Ila nataka kuuliza swali mbona nyingine zilizokopiwa hapa Tanzania toka nje hazikuzungumziwa kama Mzee wa Swagga? Nadhani jibu ni sababu JB ameitendea haki filamu hiyo, ila tusiende huko

Jambo jingine, mnapokaa kulaumu mjue kazi ya kuwapa watazamaji kitu wanachotaka kila siku na kuwafanya wakupende si suala dogo, tunaumiza vichwa mchana na usiku. JB si kwamba namfagilia sababu namuandikia ila huwa anaumia sana kutafuta story mpya na ukweli hata mimi nateseka sana kutengeneza vitu vipya na ukitazama mtu huyu mmoja atengeneze filamu 6 au 7 kwa mwaka na zote mzipende na kufurahia inahitaji kujitoa kwa hali ya juu. Nikiwa kama mwandishi kihalali nahitaji kuandika script 2 tu kwa mwaka ili nitoe vitu vikali, unapoelemewa na mzigo ni rahisi kuharibu kazi na kwa kuwa tunajitahidi (mimi na JB) kuwapa mnachopenda basi huwa tunatafuta kila njia kutowakwaza mashabiki, naomba mtuhurumie nasi kwani mazingira ya kazi ni magumu mno.

Kwa haya niliyoandika ningependa kuwaambia tusiwe watu wa kulaumu na kuhukumu, mimi kuproduce filamu yangu mwaka jana kumepunguza kujitoa kwangu kuandaa filamu kali za JB, mimi ndiye wa kulaumiwa na si JB. Na kwa niaba ya mashabiki wa JB nawaomba radhi kama kwa namna moja au nyingine mmejisikia vibaya ila kwa niliyoeleza mtaungana nami kuwa si dhambi kufanya hivyo inapobidi na tushirikiane kupeleka gurudumu hili mbele. Mimi ndiye mwandishi bora wa script na natambua jukumu langu kama mwandishi simkingii kifua JB bali nasimamia kile ninachokifanya kama Professional. Naomba tuache kuongea na tushirikiane kuboresha filamu zetu.”

Post a Comment

 
Top