Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, (pichani) ametangaza majina 99 ya Watanzania wanaodaiwa kuficha mabilioni ya Shilingi katika benki moja nchini Uswis.
Majina hayo ameyatangaza katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam jana, ambapo amesema majina hayo ameyapata hivi karibuni katika taarifa ya benki moja inayofahamika kwa jina la HBC yenye makazi yake nchini humo.
Zitto ambaye hata hivyo, hakuyataja majina hayo kwa kile alichodai kuwa anabanwa kisheria, ameyakabidhi kwa vyombo vya habari ili kuhakikisha kila Mtanzania anafahamishwa.
Kwenye mkutano huo ambao ulihudhuriwa na maelfu ya watu, alipata nafasi ya kukitambulisha chama hicho kwa wakazi wa jiji hilo.
Alisema katika majina hayo, kuna wale waliohusika katika kashfa ya rada, hivyo ni dhahiri pesa nyingi zilizohifadhiwa zinatokana na vitendo vya ufisadi.
“Katika utaratibu wa kuweka fedha lazima watu hawa waombe kibali Benki kuu, lakini kutokana na serikali kuwa kimya licha ya kelele zetu, ni bora turudi kwenu,” alisema.
Alisema Mwembeyanga ni sehemu ya kihistoria kwani mwaka 2007 ndipo kulitajwa orodha ya mafisadi na jana ameamua kurudia historia hiyo.
Orodha hiyo yenye kurasa nne ilionyesha namba za akaunti ya watu hao, majina na tarehe ya kuzaliwa, ambapo mengi ni ya wafanyabiashara wakubwa wenye asili ya Asia na Watanzania.
Alisema kuwa wameamua kufanya hivyo kwa kuwa serikali imekuwa kimya licha ya majina kama hayo kupatiwa baada ya jaji mmoja wa Ufaransa kugundua kwamba kuna majina ya watu wenye akaunti zao kwenye benki ya Uswis.
Alisema hiyo ni benki moja, lakini kuna benki nyingi za nje ambazo Watanzania wameficha fedha.
“Tunachotaka serikali ichunguze kipi ni halali na haramu kwa kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara walipeleka fedha huko kihalali," alisema.
Zitto alisema tangu wapeleke vithibitisho hivyo, sasa ni miaka miwili na miezi sita imepita lakini serikali haijafanya chochote, kutoa majibu wala kupeleka bungeni suala hilo ili Watanzania waelewe.
Alitoa mfano katika vituo vya jeshi ambavyo Watanzania wameweka Paundi milioni 40,000 sawa na Sh. Trilioni 1.3 na Uswis ni dola milioni 305.
Alisema chama chake kimekuja kama chama mbadala kuleta mageuzi na misingi yake inafuata ile ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyoacha ya kuwa na maadili ya viongozi.
Alishangaa kitendo cha baadhi ya vyama kumuita msaliti, na kwamba katika shughuli za kisiasa hakuna usaliti kwa sababu wanasiasa wanapogombana baadaye huwa wamoja.
Alitoa mfano baadhi ya wabunge Dodoma waliitwa mashoga lakini sasa hivi ni wamoja.
Pia alitoa mfano wa James Mbatia, aliitwa mbunge wa viti maalum lakini sasa hivi wameungana na kuendeleza siasa. Alisisitiza kuwa katika chama chao wameweka sheria kila mtu anapojiunga lazima atangaze mali zake.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment