Bibi harusi Doroth Msuya aliyetoroka saluni
akipambwa saa tatu kabla ya kufungwa kwa harusi
yao na kumwacha solemba bwana harusi, Joseph
Machange amepatikana jijini Arusha.
Polisi mkoani Kilimanjaro imesema binti huyo
hakutekwa nyara kama ambavyo wanafamilia
walitoa taarifa Kituo cha Polisi Himo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence
Ngonyani alisema jana kuwa uchunguzi uliofanywa
umethibitisha kuwa bibi harusi huyo hakuwa
ametekwa nyara.
“Polisi walifungua jalada la uchunguzi na ilibainika
kuwa taarifa za kutekwa zilizokuwa zimetolewa
hazikuwa na ukweli, bali aliondoka kwa kupanda
pikipiki,” alisema.
Kamanda Ngonyani alisema uchunguzi huo ulibaini
kuwa wakati akipambwa, aliomba kwenda
kujisaidia na baadaye kuomba apelekewe kanga na
‘tishu’ lakini akatumia mwanya huo kuondoka,”
alisema.
Alisema uchunguzi huo umebaini kuwa baada ya
kupanda pikipiki ilimpeleka hadi kituo cha mabasi
na alimlipa dereva wa bodaboda kisha alipanda
gari la abiria lililompeleka hadi mjini Moshi.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita saa 6.30
mchana eneo la Lole huko Mwika, Moshi wakati
bibi harusi huyo alipotoroka saluni akimwacha
mpambe wake akiendelea kupambwa.
Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe saa tisa alasiri katika
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Usharika wa Lole Dayosisi ya Kaskazini na baadaye
sherehe ingefanyika katika Ukumbi wa Mamba
Complex.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa familia ya
Machange, zilieleza kuwa Doroth alipatikana juzi
baada ya kuonekana akiweweseka, kisha
akapelekwa hospitali ya Seliani kwa matibabu.
Ndugu wa karibu wa familia ya Machange ambaye
aliomba jina lake lisitajwe, alisema kulikuwa na
kikao kilichokuwa kikiendelea kati ya familia ya
Machange na Msuya.
“Jana (juzi) tulipigiwa simu na kuelezwa kuwa
Doroth amepatikana Arusha lakini yuko kama
hajielewielewi na hajui nini kimetokea,” alisema.
Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo, zinadai
kuwa bibi harusi huyo alikuwa ametaka harusi hiyo
iahirishwe na ombi hilo alilitoa zaidi ya mara 10
bila kueleza sababu.
Source:Mwanachi
Post a Comment