Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameungana na wadau wengi wa amani nchini, kutaka viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri amani ili kunusuru Taifa na matukio ya kuhatarisha amani ambayo yanaonekana kuinyemelea nchi.


Mkapa alisema hayo jana jijini hapa alipozungumza na maaskofu, mapadri na uongozi wa Chuo Kikuu cha Weill Bugando wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo la maktaba ya chuo hicho, itakayopewa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kama ishara ya kutambua mchango wake katika sekta ya elimu wakati wa uhai wake.
Alisema siku za hivi karibuni, Taifa limeshuhudia matukio ya kuhatarisha amani yakiwamo yale ya waumini kuvamiwa katika nyumba za ibada, ambapo aliwataka viongozi wa dini kuungana na Watanzania kuombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.
"Bila amani ni dhahiri nchi itaingia kwenye matatizo, rai yangu kwa wananchi waendelee kuombea viongozi wa dini waendelee kuhubiri amani na upendo katika Taifa letu, naomba viongozi wetu wa dini waendelee kuhubiri amani," alisema. 
Aliongeza kuwa uwepo wa amani katika Taifa lolote duniani ni muhimu, kwa sababu itasaidia kuendelea kufanyika shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa imara, kinyume na hapo mipango ya nchi haitatekelezwa kikamilifu amani ikitoweka.
Aliushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Weill Bugando kwa kuamua kujenga maktaba hiyo, ambayo alisema yeye wakati anasoma wazazi wake walimtaka asomee upadri, udaktari au ualimu.
"Licha ya wazazi wangu kunitaka niwe padri, daktari au mwalimu, nilijikuta nikisomea fani zingine ikiwamo ya uandishi wa habari, lakini leo nafurahi kuungana nanyi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo hili muhimu kwetu sote," alisema. 
Akiwa hapa, jana usiku Mkapa alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi wa jengo hilo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Padri Cleophas Mabula, alisema jengo hilo limejengwa kwa lengo la kutekeleza azma ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania la utoaji elimu bora katika fani za afya.
"Lakini pia ni kutokana na ongezeko la wanafunzi chuoni hapa, ambapo kwa sasa chuo kina wanafunzi 1,536 kutoka 10 wakati kinaanzishwa mwaka 2003, hivyo tumeona kuna mahitaji ya maktaba kubwa na ya kisasa," alisema. 
Mabula alisema jengo hilo linatarajiwa kuwa Kituo cha kujifunzia, huku likiwa na maktaba, kituo cha Tehama, maabara zitakazokuwa zikiendeshwa kwa teknolojia ya Habari na Mawasiliano na huduma nyingine pia. 
Jengo hilo linajengwa na mkandarasi Shirika la Uchumi la JKT-SUMA, kwa gharama ya Sh bilioni 3.4 fedha za ndani, huku kazi ya usimamizi ikifanywa na kampuni ya MK ArchPlan Associates ya Mosh
 

Post a Comment

 
Top