Wanajeshi saba wa Tanzania, ambao ni miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa, cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wanadaiwa kuwa wameuawa.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kwamba wanajeshi hao wa Tanzania, wamekufa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaopigana na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, miili yao wanajeshi hao bado ipo nchini Sudan ikisubiri taratibu za kusafirishwa kuletwa nchini.
Hii ni mara ya kwanza kuripotiwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kufa kwa wakati mmoja.
Agosti mwaka jana wanajeshi watatu wa Tanzania huko Darfur waliripotiwa kuuawa kwenye tukio kama hilo.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
, Kanali Kapambala Mgawe alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu vifo vya wanajeshi wa Tanzania huko Darfur, alisema kuwa naye amesikia, lakini hana taarifa rasmi kwa mujibu wa taratibu za kiofisi.
Hii ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa katika Jimbo la Darfur, ambapo Agosti mwaka jana, Kanali Mgawe alinukuliwa na vyombo vya habari akithibitisha kutokea kwa vifo vya askari watatu ambao gari lao lilizolewa na maji walipokuwa wakivuka mto uliokuwa umefurika maji.
Kanali Mgawe aliwataja askari hao kuwa ni Sajini Julius Chacha, Sajini Anthony Daniel na Koplo Yusuph Said na kwamba askari wengine walinusurika baada ya kuogolea.
Tanzania ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani jimbo la Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa kulinda amani katika jimbo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Tanzania wametawanywa kwenye miji ya Khor Abeche na Muhajeria kusini mwa Darfur.
Aprili mwaka huu Tanzania ilipeleka wanajeshi wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupambana na kikundi cha waasi wa nchi hiyo M23 kinachopigana kuiangusha serikali ya DRC.
Majeshi ya Tanzania yalipelekwa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania inaungana na nchi za Afrika Kusini na Malawi kukamilisha kikosi cha wanajeshi 3,000. Tanzania imepeleka wanajeshi 850.


“Tanzania imekuwa ikijihusisha na misheni za amani, mafunzo na ushauri kwa nchi nyingi,” alinukuliwa Kanali Mgawe, na kueleza kuwa majeshi ya Tanzania yamekuweko katika vikosi vya kulinda amani huko Lebanon, Darfur, Sudan Kusini, Visiwa vya Comoro na Liberia. Liberia waliuawa wanajeshi wa Tanzania 11.
“Tanzania daima haiendi kwa nchi yeyote bila ya kuombwa na nchi hiyo au kutoka Umoja wa Mataifa,” alisema.

MWANANCHI

Post a Comment

 
Top