MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Jumanne Tevez, mkazi wa Dar es Salaam, amefanyiwa unyama baada ya kudaiwa kukatwa uume wake na wenzake.
 
Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zilisema kuwa Tevez, amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini akipatiwa matibabu.

Chanzo chetu hicho ambacho kipo karibu na familia ya mfanyabiashara huyo, kilieleza kuwa taratibu zinafanywa ili mke wake pamoja na kaka yake waweze kusafiri kwa ajili ya kwenda kumchukua.
 
“Hizo taarifa ni za kweli kabisa na hivi ninavyokuambia mke wake na kaka yake wanatarajia kuondoka kesho ili wakamchukue. Amelazwa katika hospitali moja huko Afrika Kusini na hali yake si mbaya sana.
 
“Yule jamaa kama unavyojua alikuwa mtu wa dili wa muda mrefu, hivyo inawezekana alitofautina na wenzake ndio maana wakamfanyia kitu mbaya, si unajua hawa jama wa poda (dawa za kulevya), humalizana wenyewe tu,”  kilisema chanzo hicho .

Picha  tulizofanikiwa kuzipata, zilimuonyesha mfanyabiashara huyo akiwa amevuliwa nguo zote huku akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni.

Tevez, anadaiwa kufanyiwa unyama huo baada ya kuwadhulumu wafanyabiashara wenzake wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Habari zinadai kuwa, mfanyabiashara huyo alifanyiwa unyama huo, Afrika Kusini baada ya kubainika kuficha dawa hizo.

Mfanyabiashara huyo anadaiwa kuficha mzigo aliopewa kutoka Afrika Kusini kuuleta Tanzania na kwamba baada ya kufika nchini, aliwaeleza wenzake kuwa mzigo huo umepotea.

Maelezo hayo yalionekana kuwaudhi waliompa mzigo huo, ndipo walipomuita Afrika Kusini, ambako baada ya kufika, waliamua kumfanyia unyama huo.

Picha mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinamuonyesha Tevez, akiwa na jeraha mgongoni, tumboni na jicho lake la mkono wa kushoto.

Mfanyabiashara huyo alijipatia umaarufu mkubwa jijini Dar es Salaam, baada ya kufunga ndoa na msanii maarufu wa muziki wa taarab, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ ama jike la Simba.
  

Katika nyimbo mbalimbali alizokuwa akiimba, Isha anasikika akimtaja mwenza wake huyo wa zamani waliyetengana.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema haijapata taarifa za kuteswa kwa mfanyabiashara huyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, amesema wizara haina taarifa hiyo na kwamba wataendelea kuzifuatilia kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
 
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Godfrey Nzoa, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipo hewani muda wote.

Post a Comment

 
Top