Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa
sana na tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur,
Sudan.
Kwa
hakika, Rais amesikitishwa sana na kitendo hicho ambako wanajeshi
wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi wa Sudan na ametuma salamu
za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kwa
familia za wafiwa wote.
Aidha,
Rais Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji
wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa
Tanzania. Rais pia anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia
katika tukio hilo waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya
ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika
salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis
Adolf Mwamunynge na familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu
amesema:
“Sina
maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu
makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao
katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa
Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu
kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”
Rais
Kikwete ameongeza kumwambia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za
wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba
hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari
mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi
katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi
iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu
heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza
Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa.
Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa
wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “
“Aidha,
kupitia kwako, nawatuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na
wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao
katika kuomboleza. Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa
Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo
wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Vile vile kwa pamoja
tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu. Amina.’
Kwa
walioumia, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia
na Watanzania wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio
hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na
shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.”
Vijana
hao waliopoteza maisha yao na walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na
ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa
kijeshi katika Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara
waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa
tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai 13, 2013
Post a Comment