Mahakama ya kikatiba nchini Uganda imefuta sheria kali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja, iliyotiliwa saini na rais Yoweri Kaguta Museveni mwezi Februari mwaka huu,ikisema kuwa wabunge walioidhinisha sheria hiyo hawakutimiza idadi iliyokua inahitajika.
Jaji Steven Kavuma aliiambia mahakama hapo jana kuwa Sheria hiyo ni "batili," kwa kuwa mchakato wake ulikiuka katiba, kwa kupita bila Kiwango stahili cha watunga sheria.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelezea uamuzi huo kama "ushindi kwa utawala wa sheria" na kutuma salamu za pongezi kwa wale wote waliochangia kufutwa kwa sheria hiyo hasa watetezi wa haki za binadamu nchini Uganda ambao hawakukaa kimya, na wakati mwingine wakijiweka katika hatari kubwa kutokana na suala hilo.
Sheria hiyo imekua imepiga marufuku mapenzi ya watu wa jinsia moja na kuwataka raia wa Uganda kuwafichua watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ushoga ambapo waliobainika kujihusisha walikabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha jela, adhabu ambayo ililalamikiwa na jumuiya ya kimataifa.
Aidha wafadhili wengi wa Uganda ikiwemo Marekani walifuta baadhi ya misaada waliyokua wakiitolea serikali ya nchi hiyo baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo.
Mchungaji Martin Sempa, anaepinga ushoga, amesema Marekani itasababisha Uganda kukumbwa na laana kama ile ya Sodoma na Gomora, akilaani vikwazo viliyochukuliwa na Marekani dhidi ya Uganda kufuatia kupitisha sheria dhidi ya ushoga.
Kutoka: Kiswahili rfi
Post a Comment