BAADA ya utata wa uhalali wa baba wa mtoto wa Mwimba Injili maarufu Bongo, Flora Mbasha kutawala kwenye magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii, hatimaye jipu limepasuka baada ya baba mdogo wa Flora, aliyejitambulisha kwa jina moja la Kisekwa kufunguka kwamba mtoto huyo ni damu halali ya Mbasha, Risasi Mchanganyiko lina kauli yake kuthibitisha hilo.



NI MAHAKAMA YA ILALA
Kisekwa alifunguka hayo juzikati katika Mahakama ya Ilala jijini Dar alipokuwa amekwenda kusikiliza kesi ya aliyekuwa mume wa Flora, Emmanuel Mbasha kudaiwa kumbaka shemeji yake ambapo alisema anamshangaa Mbasha kushindwa kukiri ukweli ulio wazi kwamba mtoto ni damu yake wakati moyoni anautambua.

TUJIUNGE NA KISEKWA
“Inakuwaje Mbasha anashindwa kukubali ukweli kwamba mtoto ni wake wakati anatambua fika kwamba ujauzito ni mali yake kabla hata ya mgogoro wao? Ndugu wote tulikuwa tunajua hilo, upande wetu na hata kwao. Mbona hakuikataa tangu kipindi hicho?

Mgogoro wao ulikuwa wa mambo ya kawaida ya kifamilia, haukuhusiana hata kidogo na Flora kuchepuka wala nini, tangu mwanzoni mwa mgogoro wao wakiwa wanaishi pamoja wameshaitwa mara tatu katika ofisi za Ustawi wa Jamii na alielezwa kuwa mkewe ni mjamzito, akifahamu ni mali yake na akaonywa kuwa kitendo cha kuendekeza migogoro ya mara kwa mara kinaweza kumletea matatizo mkewe na kichanga kilichokuwa tumboni, mbona hakubisha? Tulikuwa tukijadili matatizo yao na kila mmoja kuweka hoja zake mezani, hakuna kati yao aliyehusisha mgogoro huo na suala la kuchepuka,” alisema Kisekwa.
KIAPO CHATAJWA
Kama hiyo haitoshi, kuonesha ana uhakika na anachokizungumza, Kisekwa alimtaka Mbasha ajiapize kwa kushika kitabu kitakatifu cha Biblia kama ana mashaka na ukweli aliouzungumza.

AKERWA NA MADAI YA GWAJIMA
Mzazi huyo alisema anakerwa zaidi jinsi ambavyo Mbasha amewahi kukaririwa akimhusisha mkewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwamba ni baba wa mtoto huyo.
“Anamsingizia tu baba wa watu (Gwajima) maskini ya Mungu kwa vile hapendi kuona anavyomsaidia Flora, lakini ukweli Gwajima sisi ni ndugu yetu, mimi G ananiita baba mdogo kama anavyooniita Flora,” alisema Kisekwa.


MBASHA ANASEMAJE?
Wanahabari wetu walipomtafuta Mbasha kuhusiana na ukweli kwamba kichanga ni mali yake, hakutaka kukubali wala kukataa zaidi ya kupinga suala la ujomba wa Flora na Gwajima.
“Flora aseme ukweli, ujomba wa yeye na Gwajima umetoka wapi? Hilo tu ndiyo nataka alifafanue kwa undani maana wajomba zake wote mimi nilitambulishwa wakati ninamuoa,” alisema Mbasha.

Mwandishi: Kuhusu ukweli kwamba mtoto ni wako unazungumziaje?
Mbasha: Hilo litajulikana tu lakini mimi nataka kujua ujomba wake na Gwajima umetoka wapi? Hapo tu.

TUJIKUMBUSHE
Mbasha na Flora ambao waliishi kwenye ndoa na kufanikiwa kupata mtoto mmoja, mwaka jana walifikia hatua ya kutengana na kila mmoja kuishi kivyake baada ya kushindwa kutatua mgogoro wao wa muda mrefu wa kifamilia.

GPL

Post a Comment

 
Top