JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limewatia mbaroni watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuwa na asili ya Somalia katika msako unaoendelea dhidi ya kundi la wahalifu wa silaha mkoani Tanga.


Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mjini hapa, kimeiambia Mpekuzi kuwa watu hao walikamatwa jana saa 5 asubuhi katika eneo la Kijiji cha Amboni Mafuriko, baada ya kuonekana katika eneo hilo wakiwa wanashangaa na hawajui wanakokwenda.

Baada ya kuonekana kwa watu hao, wananchi wa kijiji hicho kilicho jirani na Kijiji cha Mleni ambako kundi la wahalifu wa silaha lilijificha, walitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kuwatia mbaroni.

“Ni kweli leo (jana) saa tano asubuhi huku eneo la Kijiji cha Amboni Mafuriko kuna watu wawili wenye asili ya Somalia walikamatwa baada ya wananchi kuwaona na kuwatilia shaka, na hivyo kufanikisha kukamatwa,” kilisema chanzo hicho.

Wakati huohuo, jeshi hilo linawashikilia watu wawili ambao ni wafanyabiashara na waumini wa dini ya Kiislamu wa Jumuiya ya Answar Suni mkoani hapa kwa tuhuma za kuhusishwa na tukio la kufadhili vikundi vya uporaji wa silaha dhidi ya polisi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, ndugu wa watuhumiwa hao walidai ndugu zao wamekamatwa na polisi siku tatu zilizopita.

“Kuna ndugu zetu wawili wameshikiliwa kwa mahojiano kwa zaidi ya siku tatu na hatujawahi kuwaona kila tukiwapelekea chakula na dhamana imekataliwa, hivyo hali hiyo inatupa wasiwasi mkubwa,” alisema mmoja wa ndugu wa watuhumiwa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mbali na matukio ya kukamatwa watu hao, hali ya ulinzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo imeimarishwa, hasa katika wodi ambayo askari waliojeruhiwa kwenye tukio la Amboni wamelazwa wakiendelea na matibabu.

Mpekuzi  ilimpotafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraser Kashai pamoja na Kamishna Mkuu wa Operesheni na Mafunzo nchini, Paul Chagonja, wote walisema wapo katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Post a Comment

 
Top