Rubani mmoja wa kike wa helikopta amepongezwa kama shujaa baada ya kuanguka nayo ardhini kutoka umbali wa futi 3,000 katikati ya jiji lenye pilika nyingi bila kusababisha madhara yoyote makubwa nchini Hawaii.
Julia Link, mwenye miaka 30, alikuwa akiendesha ndege hiyo nyepesi akiwa na abiria wake Karl Hedburg, mwenye miaka 71, katika safari ya upigaji picha ndipo ghafla injini ikazimika juu ya mji mkuu wa Honolulu.
Helikopta hiyo ilijibamiza kwenye mtaa, na kutua jirani kabisa na jengo moja kubwa na Chuo Kikuu cha Hawaii Pacific majira ya Saa 9:30 mchana, lakini kimiujiza hakuna yeyote aliyejeruhiwa vibaya.
"Kila kitu kilionekana kawaida katika ndege hiyo," alisema Julia. "Ghafla ikawa kimya kabisa. Injini ikazima.
"Kwanza, nilifikiri masihara. Nikasema, "Oh Mungu wangu! Hii ni kweli!" Futi elfu tatu si wakati wa kufikiria vitu. Tulijaribu hivi wakati wote."
Akituliza kichwa, Julia hatimaye aliweza kuwasiliana kwa redio na Idara ya Zimamoto ya Hawaii kuwatahadharisha kuhusu kuanguka kwake huku helikopta hiyo ikiwa inadondoka kutoka angani.
Baada ya kuanguka kando ya Mtaa wa Fort huko katikati ya Honolulu, helikopta hiyo hatimaye ilijikita kwenye gari lililoegeshwa na kuishia kutulia katikati ya barabara hiyo.
Hedburg alitibiwa majeraha yake madogo kichwani, lakini mbali na hiyo hakuna yeyote aliyejeruhiwa vibaya.
"Nilisali kabla ya kuruka na nilimaanisha, Mungu atatushusha chini salama," alisema Hedburg.
"Hakika nimesikitika kiasi kupoteza ndege mpya kabisa! Tulivyotua ilikuwa safi sana, nalazimika kusema. Nina furaha kila mmoja alitoka akiwa hai," aliongeza Julia.
Kikosi cha zimamoto walisema ujuzi pekee wa rubani ndio uliowezesha kuepusha balaa kubwa.
Helikopta hiyo ilikuwa ikimilikiwa na kampuni ya kukodisha helikopta ya Mauna Loa lakini mwakilishi wa kampuni hiyo hakuweza kupatikana mara moja kuweza kutoa maoni yake.
Taarifa za awali zinaashiria kwamba helikopta hiyo Robinson R22 Beta ilikuwa na tatizo la injini, alisema Allen Kenitzer, msemaji wa Mamlaka Kuu ya Anga.
Post a Comment